Aveline Kitomary, Dar es Salaam
Mmoja wa pacha waliotenganishwa nchini Saudi Arabia na kurejea nchini Agosti 30, mwaka huu, Anisia Bernard, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Septemba 3.
Daktari aliyekuwa akiwahudumia watoto hao, Dk. Petronila Ngiloi amesema chanzo cha pacha huyo kupoteza maisha ni baada ya kutapika kwa muda mrefu na matatizo kwenye utumbo hali iliyosababisha kupoteza maji mengi na kushindwa kula chakula.
“Tangu walivyotoka safarini mmoja alionekana hakuwa na hali nzuri na tulivyotoka uwanja wa ndege tulikwenda moja kwa moja hospitali kumfanyia uchunguzi baada ya kuanza kutapika na kupandisha homa, hali hiyo iliyosababisha ashindwe hata kula lakini tukiwa kwenye ndege alikuwa anatapika.
“Hata hivyo vipimo ulioonesha kulikuwa na hitilafu kwenye utumbo ulikuwa umejikunja tulimfanyia upasuaji lakini hali iliendelea kuwa mbaya na baadaye kupoteza maisha akiwa ICU,” amesema Dk. Ngiloi.
Pacha hao Anisia na Melnes, walizaliwa January 29, mwaka jana wakiwa wameungana huko Misenyi mkoani Kagera na kupelekwa nchini Saudi Arabia kwa ajili ya kutenganishwa kazi iliyofanikiwa na kurudishwa nchini Agosti 31, mwaka huu.