JUBA, SUDAN KUSINI
ALIYEKUWA Mkuu wa Majeshi Sudan Kusini, Paul Malong, ameunda kundi lake jipya la waasi.
Malong ambaye alitimuliwa kutoka wadhifa huo na Rais Salva Kiir mwaka jana, amechukua hatua hiyo wakati nchi yake ikianza tena mazungumzo ya amani mjini Addis Abba, Ethiopia.
Mazungumzo hayo yanalenga kufikia makubaliano ya kuachiliwa kwa Makamu Rais Riek Machar, ambaye kwa sasa yuko katika kizuizi cha nyumbani nchini Afrika Kusini.
Malong, ambaye amekuwa akiishutumu Serikali kwa rushwa na kuifilisi nchi, alisema kundi lake hilo litakuwa na jukumu kubwa la kuiondoa Sudan Kusini kutoka sintofahamu na kuielekeza katika demokrasia na maendeleo.
Serikali ambayo bado haijasema lolote kuhusu kuundwa kwa kundi hilo, inapigana na vikundi kadhaa vya waasi nchini hapa.
Inaarifiwa wakati Malong alipokuwa ana wadhifa wa mkuu wa majeshi, alikuwa akituhumiwa na Umoja wa Mataifa (UN) kuratibu mashambulizi ya kikabila dhidi ya raia na tuhuma hizi ni sababu ya kuondolewa kwake.
Wakati hayo yakijiri, inaarifiwa mapigano yanaendelea nchini hapa baina ya vikosi vya Serikali na vikundi vya waasi licha ya mpango wa amani uliosainiwa mwaka 2015.