Na ASHA BANI, Dar es Salaam
KUTOKANA na mauaji yanayoendelea mkoani Pwani, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo ambaye alitarajia kufanya ziara na kuzungumza na wazee wa mkoani humo ameahirisha ziara yake.
Habari zilizopatikana juzi jioni zilieleza kuwa Jenerali Mabeyo alitarajiwa kwenda Wilaya ya Kibiti kwa  mazungumzo na wazee kuhusu mauaji hayo.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Gullamuhusein Kifu aliliambia gazeti hili kwamba ziara hiyo imeahirishwa kwa vile Jenerali Mabeyo alikuwa anakabiliwa na majukumu mengine ya ofisi.
“Ameahirisha ziara yake ni kweli alitakiwa kuja lakini kutokana na sababu mbalimbali za ofisi na kuwa na kazi nyingine   atatujulisha tena muda wa kuja huku,’’alisema Kifu.
Juzi mauaji hayo yaliendelea baada ya akari wawili wa usalama barabarani kuuawana watu wasiojulikana wakiwa katika eneo la Bungu B, Jaribu mpakani.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amekwisha kulitembelea eneo hilo na  kuzungumza na wananchi  na viongozi.
Mkuu wa Jeshi la Polisi   (IGP) Simon Sirro naye amekwisha kulitembelea eneo hilo na kuahidi  kukomesha mauaji hayo.
lVilevile, juzi akiwa katika ziara yake mkoani Pwani, Rais Dk. John Magufuli, pamoja na mambo mengine, aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwafichua wauaji.
Alisema   kuendelea na mauaji hayo kunaweza  kurudisha nyuma maendeleo wilayani humo na kuogopesha wawekezaji.