Derick Milton, Busega
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Busega Mkoani Simiyu, Anderson Njiginya pamoja na maofisa ardhi wakiongoza na Ofisa Ardhi wa halmashauri hiyo wametakiwa kurejesha mara moja kiasi cha shilingi milioni 55.58 ambazo zinadaiwa malipo hewa.
Mkurugenzi huyo pamoja na watalaamu hao wanadaiwa kuhidhinisha kiasi hicho cha pesa kwenda katika mradi wa upimaji na urasimishaji viwanja 3700 vilivyopo katika kata za Kiloleli, Kabita, Mwamanyiri na Mkula.
Kiasi hicho cha fedha kinadaiwa kulipa majina hewa ya wananchi walioingizwa ndani ya mradi,kulipa posho watumishi wasiohusika na shughuli za mradi pamoja na kulipwa zaidi ya mara moja katika uendeshaji wa shughuli za mradi huo kwenye eneo moja.
Hayo yamebainika leo kwenye kikao maalumu cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo wakati Katibu tawala wa mkoa huo Jumanne Sagini akiwasilisha ripoti ya kamati maalum iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza matumizi ya fedha hizo ambazo matumizi yake yalikuwa yakifanyika kinyume na utaratibu.
Sagini amesema kuwa katika uchunguzi huo,kamati iliwabaini watumishi hao kuhusika moja kwa moja na ubadilifu huo na amewataja kwa majina kuwa ni Mkurugenzi wa Halmashauri Anderson Njiginya ,Agustine Kitau mhasibu wa mradi, Magesa Magesa afisa ardhi wa Wilaya pamoja na Raymond Mahendeka.
“kwa masikitiko makubwa wenzetu waliopewa dhamana na mamlaka ya kusimamia miradi ya serikali na wananchi wanatuangusha na badala yake wanajinufaisha wenyewe kwa fedha za serikali…na wahusika wote wanatakiwa kurejesha fedha hizo pamoja na kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” amesema Sagini