Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imepogezwa kutokana na jitihada inazozifanya za kutoa elimu na mafunzo kwa jamii ili kukuza uelewa wa wananchi inaowahudumia.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Temeke,Elihuruma Mabelya, alipotembelea banda la BRELA Mei 23, 2023 katika “Tamasha la kijana Janjaruka na Fursa” linaofanyika katika viwanja vya Zakhiem- Mbagala, jijini Dar es Salaam.
Akiwa katika banda la BRELA Mkurugenzi huyo ameshuhudia muitikio wa wananchi wa Temeke katika kupata elimu na huduma za papo kwa papo zinazotolewa na Taasisi katika tamasha hilo.
Awali, Mkurugenzi huyo alielezwa na Afisa Usajili Mwandamizi wa BRELA, Nassoro Mtavu namna BRELA inavyoshiriki kutoa elimu kwa umma mbali ya kushiriki kwenye matamasha na maonesho mbalimbali, kuwa ni pamoja na kutembelea taasisi za elimu ya juu na ya kati, kushiriki katika semina na makongamano pamoja na kutoa elimu kwa njia ya redio, televisheni na mitandao ya kijamii.
Mtavu amewasihi wananchi wa Temeke kutumia fursa iliyopo kwa kufika katika banda la BRELA ili kupata huduma na kutatuliwa changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wakati wa usajili katika mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao.