MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM
MAMBO yamezidi kuwa magumu kwa wachezaji wanne wa Simba wanaotuhumiwa kwa vitendo vya nidhamu walivyofanya wakati timu yao ikikabiliwa na michezo miwili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Kanda ya Ziwa.
Wachezaji hao ni Jonas Mkude, Clatous Chama, Gadiel Michael na Erasto Nyoni ambao hawakuambana na kikosi hicho Kanda ya Ziwa kuvaana na timu za Kagera Sugar ya Bukoba na Biashara United ya Mara.
Baada ya wachezaji kushindwa kusafiri na wenzao, klabu ya Simba iliwatia hatiani kwa makosa ya kinidhamu na kuburuza kwenye kamati ya nidhamu ili kutoa adhabu inayostahili.
Juzi klabu ya Simba ilitoa tamko kuwa imeshasikiliza utetezi wa wachezaji hao na kinachosubiriwa ni kumalizika kwa majukumu yao katika timu za taifa yanayowakabili ili kutoa hukumu.
Wakati wachezaji hao wakiendelea kusubiria hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji wa Soka la Kulipwa nchini (SPUTANZA), Mussa Kisoki, amepigilia msumari suala hilo kwa kusema wachezaji wamekiuka taratibu, hivyo ni ngumu kukwepa adhabu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kisoki alisema vitendo vya utovu wa nidhamu havileti picha nzuri kwa wachezaji wa kulipwa kwani haviendani na weledi wa wachezaji hao.
Alisema wao kama SPUTANZA hawatakuwa tayari kumtetea mchezaji yeyote atakayekwenda kinyume na matakwa ya mkataba wake, kwani kufanya hivyo ni kulea ugonjwa unaodidimiza soka nchini.
“Tunakemea kwa sauti kubwa vitendo hivi vya utovu wa nidhamu, tuko kinyume navyo kwa kweli, tuna dhamana ya kutetea maslahi ya wachezaji, lakini si kwa wale wanaokiuka masharti ya mikataba yao.
“Kwa jambo kama hili la akina Mkude, sisi tunasimama kuunga mkono klabu hiyo, kama ikidhibitika kweli wametenda makosa basi hatua kali zichukuliwe dhidi yao ili iwe funzo kwa wengine,” alisema.
Kisoki alisema japo kuna taarifa zinadai kuwa wachezaji hao walishindwa kuungana na timu hiyo kutokana na kutolipwa haki zao, lakini hawakupaswa kugoma kwa sababu kufanya hivyo ni kinyume na taratibu za soka la kulipwa.
“Hata kama wangekuwa wanaidai klabu, hawakupaswa kugomea mechi hizo, uzuri wachezaji wote hao wanasimamiwa na mameneja wao, hivyo kama kulikuwa na tatizo lolote wasimamizi wao walipaswa kulimaliza hilo huku wao wakiendelea na majukumu yao uwanjani.
“Lakini kama walishindwa kwenda Bukoba kutokana na mambo yao basi hawana cha kujitetea, wakumbuke wao ni waajiriwa hivyo kama walikuwa na sababu zozote basi uongozi ni muhimu kujua, kwa namna jambo lenyewe lilivyo naona wachezaji hawa wamekosea na klabu ina mamlaka ya kuchukulia hatua kali za nidhamu,” alisema Kisoki.
Tayari sakata hilo la utomvu wa nidhamu ndani ya kikosi cha Simba, limedaiwa kuelekea kumponza Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems, akidaiwa kulea ‘uonzo’.