Kisa Pyramids, Yanga yajisalimisha kwa matawi

0
868

WINFRIDA MTOI, DAR ES SALAAM

UONGOZI wa klabu ya Yanga, unatarajia kukutana viongozi wa matawi ya wanachama wa klabu hiyo ili kuweka mikakati ya kufanya vizuri katika michuano inayowakabili, ikiwamo Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga ambayo imeanza vibaya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), inatarajia kukutana na Pyramids hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho.

Wanajangwani hao wanatarajia kuanzia nyumbani kuivaa timu hiyo tajiri ya Misri, mchezo utakaopigwa Oktoba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kabla ya mchezo huo, Yanga inakabiliwa na mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbao FC, itakayochezwa Oktoba 24, 2019 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara Habari na Mawasiliano, Hassan Bumbuli, alisema kutokana na mwenendo wa timu ulivyo, uongozi wa klabu hiyo umeona ni vema kufanya kikao na matawi yao yote.

Alisema lengo ni kuweka mikakati ya michuano iliyopo mbele yao, lakini pia kujenga umoja na mshikamano, hasa kuelekea mechi za Kombe la Shirikisho na Ligi Kuu Bara.

Bumbuli alisema mkutano huo, unatarajia kufanyika wiki ijayo katika makao makuu ya klabu hiyo, Jangwani, jijini, kila mmoja aweze kutoa mchango wake wa mawazo, akiwakilisha wanachama.

“Tunataka kutengeneza mikakati thabiti, baada ya ratiba ya Kombe la Shirikisho na uwepo wa maneno mengi ya kuonyesha kuna shida katika uongozi, viongozi wa matawi wameomba mkutano huu.

“Mikakati tutakayoweka italenga pia mechi za Ligi Kuu, baada ya kuanza kupata ushindi, tunataka kuendeleza hali hiyo, hivyo ni muhimu Wanayanga wakawa kitu kimoja na kuachana na maneno ya pembeni,” alisema Bumbuli.

Alieleza kuwa baada ya mkutano huo, hawatasikia tena maneno ya mitaani, kuuzungumzia uongozi vibaya kwa sababu kila kiongozi wa tawi atakwenda kuongea na watu wake, kuwe la lengo moja.

Naye Mhamasishaji wa klabu hiyo, Antonio Nugaz, alisema hawatishwi na utajiri wa Pyramid kwa sababu wanajua mpira unachezwa uwanjani, ukizingatia Yanga ni wazoefu wa michuano hiyo.

“Tunajua (Pyaramids) ni timu ndogo ndio inaanza kushiriki michuano hiyo, lakini hatuichukulii poa kwa kuidharau, pia hatutishwi na vigezo vyake kuwa ina thamani kubwa, mpira unachezwa uwanjani.

“Mpira haujezwi kwa maneno, tunafurahi kupangiwa na timu kutoka Misri kwa sababu janja janja zao tunazijua, wakija Dar es Salaam, tutahakikisha mchezo unamalizika hapa hapa, tukienda ugenini tunafunga mjadala kwa kuwawekea ukuta,” alisema Nugas.

Alieleza kuwa kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera, ameacha program yake, watacheza michezo miwili ya kirafiki na timu ya Friends Rangers kesho na Pan Africans Oktoba 16.

Nugaz alisema baada ya michezo hiyo, timu itaondoka Dar es Salaam, Oktoba 20, kuelekea Mwanza kwa mechi yao ya Ligi Kuu na Mbao FC, kisha kurudi kujiandaa na Pyramids.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here