26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mkishindwa nipisheni – Magufuli

Pg 2Na Elias Msuya

RAIS John Magufuli amewataka makatibu na manaibu makatibu wakuu walioapishwa jana kukubali ahadi ya uadilifu wa viongozi na asiyetaka akae pembeni.

Akizungumza baada ya kuwaapisha makatibu na manaibu makatibu wakuu katika Ikulu ya Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema hakuna aliyelazimishwa kula kiapo cha ahadi za uadilifu wa uongozi wa umma, hivyo asiyetaka akae pembeni.

“Tusije tukawa tunazungumza hapa kwa ‘generalization’ (kwa ujumla), lakini kumbe si wote wanakubali hayo masharti kama vile rushwa na kadhalika, kutoa vitu kwa upendeleo… Kwa hiyo mimi niwaombe makatibu wakuu pamoja na kwamba mmeshaapa kwangu; ambaye hakubaliani na hilo asimame pembeni tu ili waliobaki waendelee,” alisema Rais Magufuli.

Naye Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alirudia kauli hiyo kwa kusema: “Mheshimiwa Rais na mimi nauliza, kuna ambaye masharti haya yanamkwaza hataki kubanwa nayo? Kama hakuna naomba tusimame kila mtu asome akitaja jina lake,” alisema Balozi Sefue.

Hata hivyo, hakuna Katibu wa Naibu Katibu Mkuu aliyejitoa kwa kukataa masharti hayo bali wengine walionekana wakitabasamu kwa tamko hilo.

Awali akisoma ahadi hizo, Kaimu Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa Umma, Waziri Kipacha, alisema ahadi hizo zimezingatia maadili yaliyoainishwa katika ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 na masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na.13 ya mwaka 1995.

Alizitaja ahadi hizo kuwa ni pamoja na; kuwa mzalendo kwa nchi na kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa mwadilifu na mfano kwa watumishi wa umma na watu wengine katika kusimamia maadili, kutotumia cheo na wadhifa kwa masilahi binafsi, kwa familia na marafiki bali kwa masilahi ya umma.

Nyingine ni kulinda na kutumia rasilimali kwa masilahi ya umma, kutekeleza majukumu na uamuzi kwa kutumia sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo kwa masilahi ya umma.

“Sitaomba, kushawishi, kutoa wala kupokea rushwa, sitaomba, kutoa wala kupokea zawadi au fadhila za kiuchumi, kisiasa za au za kijamii zisizoruhusiwa na sheria.

“Sitatoa shinikizo kinyume cha sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika utendaji wa kazi za umma. Nitatenda kazi kwa kuepusha migongano ya masilahi ya aina yoyote na endapo utatokea, uamuzi wangu utazingatia masilahi ya umma,” alisema Kipacha.

Aliendelea kusoma: “Nitatoa huduma bora kwa watu wote bila kujali misingi ya dini, siasa, ukabila undugu, ukanda, jinsia au hali ya mtu. Nitaepuka tabia ambayo inavunja heshima ya uongozi wa umma hata nitakapokuwa nje ya mahali pa kazi au nitakapoacha kazi.”

Jumla ya makatibu na manaibu Katibu wakuu 26 waliapishwa akiwemo Profesa Adolf Mkenda (Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Uwekezaji). Wengine ni Mhandisi Mussa Iyombe (Katibu Mkuu), Dk. Deo Mtasiwa (Naibu Katibu Mkuu – Afya), Bernard Makali (Naibu Katibu Mkuu Elimu) Wizara Ofisi ya Rais katika Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Wengine walioapishwa ni Mbaraka A. Wakili (Katibu Mkuu), Mhandisi Ngosi Mwihava (Naibu Katibu Mkuu) wa Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais.

Katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge, Sera, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) walioapishwa ni Erick Shitindi (Katibu Mkuu Kazi na Ajira), Mussa Uledi (Katibu Mkuu Bunge), Dk. Hamis Mwinyimvua (Katibu Mkuu – Sera).

Katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi walioapishwa ni Dk. Maria Salome Mashingo (Katibu Mkuu Mifugo) na Dk. Budeba (Katibu Mkuu – Uvuvi) na katika Wizara ya Ujenzi Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano walioapishwa ni Mhandisi Joseph. Nyamuhanga (Katibu Mkuu – Ujenzi), Dk. Leonard M. Chamuliho (Katibu Mkuu – Uchukuzi), Profesa Faustine R. Kamuzora (Katibu Mkuu – Mawasiliano) na Mary Sassabo (Naibu Katibu Mkuu Mawasiliano).

Katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi walioapishwa ni Dk. Yamungu Kayandabira (Katibu Mkuu) na Dk. Naibu Katibu Mkuu Moses Kusiluka.

Wizara ya Maliasili na Utalii walioapishwa ni Meja Jenerali Gaudence Milanzi (Katibu Mkuu), Anjelina Madete (Naibu Katibu Mkuu) na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji aliapishwa Naibu Katibu Mkuu Mhandisi, Joel Malongo.

Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi walioapishwa ni Manaibu Katibu wakuu Profesa Simon Msanjila na Dk. Leonard Akwilapo.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto walioapishwa ni Dk. Mpoki Ulisubisya (Katibu Mkuu – Afya) na Sihaba Nkinga (Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) na Wizara ya Nishati na Madini walioapishwa ni Profesa Justus Ntalikwa (Katibu Mkuu) na Manaibu Katibu wakuu Profesa James Mdoe na Dk. Paulina Pallangyo.

Katika Wizara ya Katiba na Sheria walioapishwa ni manaibu katibu wakuu Suzan Paul na Amon Mpanju huku Wizara ya Mambo ya Ndani, Jaji Meja Jenerali Projest A. Rwegasira (Katibu Mkuu) na Naibu Katibu Mkuu Balozi Hassan Simba Yahaya.

Wizara ya Fedha na Mipango walioapishwa ni manaibu katibu wakuu ambao ni Dorothy Mwanyika, James Dotto, Amina Hamis Shaban huku Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa wakiapishwa, Dk. Aziz Mlima (Katibu Mkuu) na Naibu wake Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi.

Katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa walioapishwa ni Job Masima (Katibu Mkuu), Immaculate Peter Ngwale (Naibu Katibu Mkuu).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles