HARARE, ZIMBABWE
MKE wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Grace Mugabe, ameteuliwa kuwa kiongozi wa kitengo cha wanawake ndani ya chama tawala cha ZANU-PF.
Grace (49) atakabidhiwa rasmi wadhifa wa kuongoza kitengo hicho katika kongamano la kitaifa la chama hicho ambalo linatarajiwa kufanyika Desemba.
Kwa mujibu wa BBC, cheo hicho kitamruhusu kushiriki mikutano ya Kamati Kuu ya ZANU-PF ambayo kimsingi ndiyo yenye shinikizo kubwa la uendeshaji wa serikali.
Taarifa zaidi zinadai kuwapo kwa mivutano na taharuki kubwa ndani ya chama kufuatia kuzorota kwa afya ya Rais Mugabe.
Kwamba hadi sasa haijulikani ni nani atakayemrithi kiongozi huyo mwenye umri mkubwa zaidi katika marais wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.
Wawili hao kabla hawajafunga ndoa mwaka 1996, walikuwa wanafanya kazi pamoja, ambapo Grace alikuwa msaidizi wa Mugabe.