PATRICIA KIMELEMETA Na CHRISTINA GAULUHANGA – DAR ES SALAAM
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amesema mjadala wa kuboresha sekta ya elimu nchini ulikuwa ni kipaumbele chake tangu alipokuwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Lowassa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema wakati akiwa Waziri Mkuu, alianzisha na kusimamia ujenzi wa shule za kata nchini, ambazo sasa zinaonekana kutelekezwa kama watoto yatima.
Kauli ya Lowassa imekuja siku moja baada ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, kutaka uwepo mjadala mpana kuboresha sekta ya elimu nchini.
“Nimesoma na kusikia Rais Mkapa akitaka kuwepo mdahalo wa kitaifa juu ya kushuka kwa elimu nchini, lakini hiyo ndiyo ilikuwa ajenda yangu ya kwanza tangu nilipokuwa CCM.
“Nimefurahi kuona mzee Mkapa akiliibua suala hili, kwani hiyo ilikuwa ni ajenda yangu ya kwanza tangu nilipokuwa CCM na nje ya chama hicho.
“Hata katika ilani ya uchaguzi ya Chadema ambacho nakitumikia kwa sasa, elimu ndiyo ajenda kuu.
“Kama ningeshinda urais, ningeita mjadala wa kitaifa juu ya elimu ili kuangalia wapi tulipokwama na nini kifanyike na zaidi tuliahidi elimu bure kuanzia shule ya chekechea hadi chuo kikuu.
“Serikali ya CCM imekuwa ikichukua ajenda zetu bila kukiri kuwa ni ajenda zilizoko katika ilani yetu ya uchaguzi, pendekezo la Mkapa ni mlolongo huo huo wa kukwapua ajenda zetu.
“Wengi ni mashahidi wa hali duni ambayo baadhi ya shule hizo zinapitia, ikiwamo ukosefu wa majengo, hasa mabweni, vyumba vya madarasa, posho za walimu, mishahara midogo, uhamisho pamoja na bajeti ndogo ya elimu.
“Kwahiyo, hiyo si ajenda ya CCM na hawataweza kuisimamia kwa sababu wanataka kuendelea kutawala kwa hila na hawataki kuwa na taifa lililoelimika vizuri, linaloweza kuhoji.
“Tazama takwimu za uchaguzi mkuu uliopita, maeneo ambako CCM ilishinda kihalali, maendeleo yako nyuma.
“Lakini pia tumeshuhudia Watanzania wenye uwezo wa kuhoji masuala mbalimbali ya nchi kwa manufaa ya Watanzania na nchi kwa ujumla wanavyoshughulikiwa.
“Kwahiyo, lazima Watanzania wafahamu kwamba njia pekee ya kupata maisha bora ni kuiondoa CCM madarakani mwaka 2020 na kuwapigia kura upinzani ili uongozi wa nchi uweze kutekeleza kwa ufasaha na umahiri ajenda ya elimu,” alisema Lowassa.
HAKI ELIMU
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya HakiElimu, John Kalaghe, alisema suala la maboresho katika sekta ya elimu lilianza kupigiwa kelele muda mrefu, lakini Serikali ilishindwa kulifanyia kazi.
Kwa mujibu wa Kalaghe, kipindi hicho wadau wa elimu walisema mfumo wa elimu nchini hauridhishi na kwamba inahitajika mijadala ya kitaifa itakayosaidia wadau kutoa maoni yao ya nini kifanyike ili kuhakikisha Serikali inatoa elimu bora.
“Tumemshukuru Rais mstaafu Mkapa kwa kuliona hilo na kulizungumza hadharani, kwa sababu tuliwahi kupiga kelele, lakini hakuna jambo lolote lililofanyiwa kazi.
“Hivyo basi, wakati umefika kwa Serikali kuangalia suala hilo na kulifanyia kazi ili elimu inayotolewa nchini iwe bora na ya kuridhisha.
“Naamini kama kutakuwa na mijadala mipana ya sekta ya elimu, wadau watajadili kuanzia suala la ubora wa walimu, vitendea kazi na ubora wa majengo na kuangalia mfumo mzima wa utoaji wa elimu,” alisema Kalaghe.
MHADHIRI UDSM
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. George Kahangwa, alisema uwepo wa mijadala utasaidia kuondoa mifumo mibovu ya utoaji elimu na kufanya maboresho katika idara mbalimbali.
“Wakati umefika sasa kwa Serikali kushirikisha wadau mbalimbali katika sekta ya elimu ili waweze kutoa maoni yao yatakayosaidia kujenga na kuondoa mifumo mibovu ya utoaji wa elimu nchini,” alisema Dk. Kahangwa.
PROFESA BAREGU
Kwa upande wake, Mhadhiri mstaafu, Profesa Mwesiga Baregu, alisema malalamiko katika sekta ya elimu si jambo geni kwa kuwa yameanza kutolewa miaka mingi iliyopita.
“Niliwahi kufanya utafiti mdogo na kubaini kwamba masuala ya kisiasa ni miongoni mwa sababu zinazochangia kurudisha nyuma sekta ya elimu nchini.
“Kuna pengo kubwa katika sekta ya elimu kutokana na kuingiza masuala ya kisiasa na watu kuigeuza elimu na kuwa kama mtaji.
“Kwahiyo, wakati umefika kwa Serikali kuangalia suala la elimu na kuweka kando tofauti za kisiasa ili wanafunzi waweze kupata elimu bora.
“Kama haitafanyika hivyo, hatutaweza kufanikiwa na tutasababisha kudidimia kwa sekta hiyo,” alisema Profesa Baregu.
Pamoja na hayo, alisema wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, baadhi ya mikoa yenye wasomi na vyuo vingi, ndiyo waliyopigia kura vyama vya upinzani.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU
Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wiliam ole Nasha, alisema tayari Serikali imeanza mchakato wa maboresho ya sekta ya elimu nchini.
Ole Nasha, aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na MTANZANIA kwa simu.
“Maboresho hayo yataangalia mfumo mzima wa sekta ya elimu kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo vikuu na wadau mbalimbali watashirikishwa ili waweze kutoa maoni yao.
Kuna mambo mengi yanayorudisha maendeleo ya nchi yetu nyuma na baadhi ya mambo hayo ni hili la viongozi kutoshirikisha wananchi katika maamuzi wanayofanya. Mfano ni hilo tamko lililotolewa na mkuu wa mkoa wa Manyara. Angekuwa amewashirikisha wananchi wake kabla ya kutoa tamko zito kama alilotoa, angekuwa ameona wazi kwamba anachosema hakiwezekani. Tena kuwaambia wasioweza kulipa hao wafanyakazi waondoke ilhali wameshawapa chakula kwa miaka mingi wakingojea siku watapata madini wagawane sio haki. Tunamwomba waziri mkuu aingilie hili swala maana kama kweli hao wachimbaji wadogo wataondolewa halafu wafungue kesi mahakamani, serikali inaweza kujikuta inalipa mabilioni ya fidia bila sababu yoyote.