29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Mjane asimulia alivyonusurika kubakwa mtaroni

JANETH MUSHI-MONDULI

MATUKIO ya ukatili ya ubakaji na mauaji ya wanawake eneo la Mto wa Mbu wilayani Monduli, yameendelea kuumiza baadhi ya wanawake wa eneo hilo huku wengine wakidai kushindwa kufanya shughuli zao za kiuchumi wakihofia usalama wao.

Kutokana na kukithiri kwa wimbi la matukio  hayo ya kikatili, hivi majuzi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, aliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha linafanya uchunguzi wa kina na kukamata wahusika wa vitendo hivyo.

Wakati waziri akiagiza kukamatwa kwa watuhumiwa wanaotekeleza uovu huo, wahusika wamelalamikia kitendo cha watuhumiwa kuachiwa huru kila wanapokamatwa na kurejea mitaani.

Akizungumza katika mafunzo ya kupinga ukatili wa kijinsia, mmoja wa manusura wa matukio ya ubakaji na mauaji ya wanawake wilayani hapa, Prisca Richard (40)  anadai alifanikiwa kumkamata mtuhumiwa wake ila alipopelekwa kituo cha polisi hakujua kesi iliishia wapi na baadaye mtuhumiwa huyo aliachiwa huru.

Akiwa katika kikao cha elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa jukwaa la wanawake Kata ya Mto wa Mbu, ambao ulishirikisha wanawake kutoka Kata za Majengo na Migungani, mama huyo ambaye ni mjane mwenye  watoto wawili, anasimulia jinsi alivyonusurika kubakwa.

Akisimulia huku akibubujikwa na machozi, Prisca anadai siku ya tukio Desemba 11 mwaka 2017, akitokea kwenye biashara zake (kuuza sambusa), eneo la Kigongoni, mida ya saa moja kasoro, ghafla aliona mtu nyuma yake ila hakuwa na wasiwasi kwa sababu walikuwa wanapishana na watu wengi njiani.

“Mungu ni mwaminifu, siku ile nilimaliza biashara mapema kuliko siku zote, maana wakati mwingine huwa namaliza saa mbili kasoro, nakumbuka nikiwa eneo la Makwetu kuna mtu nilibaini ananifuata nyuma yangu,” anadai na kuongeza:

“Nafsi yangu ikaniambia mtu aliye nyuma yako si mzuri, lakini nikaendelea na safari yangu, baadae nafsi ikaniambia geuka nyuma yako mtazame huyo mtu, nilipogeuka akatahayari nami nikajawa na hofu, nikajiuliza, mbona tunapishana na watu saa hizi huyu atanifanya nini?

Anadai alipofika mbele kidogo, alilazimika kugeuka na yule mtu akasimama, alipoendelea  mbele zaidi  karibu na kanisa alimuona kijana anayemfahamu naye akasimama na kuanza kuzungumza naye ili aone kama aliyekuwa anamfatilia nyuma yake atamsubiri au ataendelea na safari.

“Alitupita ila baada ya hatua kama 10 hivi akasimama, akawa anaita ng’ambo ya pili ya barabara kwa sauti kubwa akisema Samweli, Samweli, moyo wangu ukashtuka.

“Kuna gari lilikuwa linapita barabara kuu nikiwa naendelea kuzungumza na yule kijana, lilipomkaribia yule mtu nikamuangalia kwa makini nakumbuka alikuwa na rasta, na alivaa sweta jeusi,” anasimulia.

Prisca anadai baada ya kumuona alijua ataweza kumkwepa kwa kuvuka upande wa pili wa barabara,  lakini alipompita hatua kama tano mbele alimshika shingoni, akadhani ni kibaka anataka kumuibia.

“Tukapambana huku akilini mwangu nikiwaza kuporwa fedha zangu za biashara.  Niling’ang’ania vihela vyangu, akaona pale ni barabarani bodaboda zinapita nyingi watamuona akashika shingo akanitupa korongoni, kuna miiba alinishindilia kwenye ile miiba ambayo hadi leo hii haijatoka yote.

“Alininyongea pale, kumbe ukishikwa shingo sauti haitoki nikaona mauti yameshanifika, nikamuomba Mungu aniokoe na roho ya mauti, kifo cha aibu ambacho kitawaumiza watoto wangu,” anasimulia mama huyo.

Anadai awali aliweza kupiga kelele kuomba msaada lakini baadae alishindwa kuendelea ila majirani wa karibu na eneo lile walishasikia na boda boda zilizokuwa zikipita,watu wakaanza kukimbilia eneo hilo ndipo mbakaji akakimbilia vichakani upande wa pili.

“Hakuchukua fedha hata kidogo, nia yake ilikuwa ni kunibaka, bahati nzuri watu waliwahi eneo la tukio. Nilishauriwa niende polisi, nilipofika nikakuta taarifa zangu zimeshafika hapo, wakaniuliza ndiye niliyebakwa, wakanipa PF3 niende hospitali.

“Nikamwambia bodaboda anipeleke, nikafika safari park  mvua ilinyesha kubwa na umeme ukakatika, nikaghairi safari ya hospitali na kuamua kwenda kwa dada yangu
nikiwa nimejaa damu, kesho yake ndio nikaenda hospitali wakanitoa miba mwilini lakini mingine ilibaki,” anasimulia.

KUKAMATWA MTUHUMIWA

Prisca anaeleza kuwa baada ya kupona alilazimika kuendelea na shughuli zake huku akimsihi Mungu amsaidie namna ya kumpata mtuhumiwa wake kwa kuwa anamkumbuka vizuri.

Anadai baada ya muda kupita, polisi wakaenda kumkamata mtoto wa jirani yake wakidai ndiye aliyetaka kumbaka, hali iliyomlazimu kwenda kuwaeleza kuwa anamfahamu mtuhumiwa wake hivyo wamuachie kijana huyo kwani hahusiki.

“Wazazi wa yule kijana walikuja kwangu wakiwa wanatetemeka, wakiniuliza mtoto wao ametaka kunibaka lini, nikawaambia sijamkamata mtuhumiwa wangu, hawakunielewa walidhani nimeenda kumtaja mtoto wao polisi, nikawaelewesha  na kuwaeleza kuwa mimi ni mzazi hivyo siwezi kumtia matatizoni mtoto wao,” anasema na kuongeza:

“Nilienda kituoni nikawaambia kwamba kijana yule hakusiki na kwamba namfahamu mtuhumiwa wangu hata kwa harufu, wakamuachia. Ila nawaambia wamama haijalishi una imani gani, ukiwa na tatizo toa sadaka inanena, nilitoa sadaka yangu kanisani na kuomba niweze kumkamata.”

Mjane huyo anadai baada ya mwezi mmoja akiwa katika shughuli zake za biashara alimkuta mtuhumiwa amekaa mahali, akalazimika kujificha na kuwashirikisha baadhi ya wanaume waliokuwa eneo lile wakamzingira, akatafuta mgambo na kumkamata kumpeleka Kituo cha Polisi Mto wa Mbu.

“Nilipofika mapokezi Polisi nikatoa maelezo yangu nikaambiwa mama andika namba ya simu tutakuita nenda, nilisubiri muda nikaona niende mwenyewe nikaambiwa wanafanya upelelezi, nikarudi tena ila nilivyorudi mara ya tatu nilifokewa.
“Nikaamua kuacha kwenda kituoni, niende kutafuta kula  yangu, wakishakuona hoi hakuna anayekuuliza una shida gani, nikawa naendelea na biashara ila nikikutana na watu wananiuliza kama najipenda, ikafika mahali wenzangu wakawa wananisaidia kuuza bidhaa
zangu ili niwahi nyumbani,”

AKIMBIA

Prisca anaeleza baada ya kuona mtuhumiwa hajafikishwa mahakamani na kuachiwa huru, alilazimika kukimbilia Mang’ola (ziwani) kwenda kupara samaki huku akiwaacha watoto wake kwa majirani kutokana na mazingira ya kule kutokuwa rafiki.

“Nilisema Mungu ninafanyaje, mtuhumiwa hayupo mahakamani wala polisi, kesi ikaishia hapo. Nilijikusanya nikakimbia ila baadhi ya wanawake waliomo humu na mtendaji wa kata walichanga nauli wakanirudisha.

“Kule kazi ilikuwa ngumu kwa sababu nilikuwa napara samaki usiku kucha, niliwaeleza bora nife na baridi kuliko kufa kifo cha aibu, nikarudi kuendelea na biashara yangu, viongozi wameshakuja wananipa imani ila hajamakatwa na wenzangu wanaendelea kuuawa.

“Naomba niwaulize waansheria, hivi aliyekufa na ambaye hajafa na anaweza kujieleza yupi anaweza kusaidia kupatikana kwa mtuhumiwa, ili kukomesha matukio haya?” anahoji na kuongeza:

“Inaniuma, nimekuja hapa kwa sababu ya kuwaonea huruma wanawake
wenzangu, natamani nikutane na Magufuli (Rais Dk. John Magufuli) maana waliobakwa ni wengi na
waliosalimika wengine hawajitokezi maana matatizo hayatatuliwi, waliokufa ndiyo
hivyo tukishazika hatufuatiliwi.”

ULEVI

Anasema ni vema uchunguzi wa mauaji hayo ungefanyika ili kujua chanzo, wapo wanaosema wanawake wa eneo hilo wanakumbana na vitendo hivyo kwa sababu ni walevi, hii si kweli.


“Binafsi  wanaonifahamu kwa undani wanajua mimi si mlevi, lakini leo amekufa Ester ambaye anajulikana alikuwa na jaribu lake la kunywa pombe, imekuwa wa mama wa Mto wa Mbu ni walevi, si wote waliouawa ni walevi.

“Imeandikwa wapi mlevi abakwe auawe? Tumedhalilishwa na kufedheheshwa wanawake wa Mto wa Mbu, mimi hivi ninavyoonekana ni mapenzi ya Mungu ndio maana naishi, hatuna haki au huyo waliyemwachia wanamuogopa?” anahoji.

Anaongeza: “Inafika mahali jua likizama narudi nyumbani na sambusa, tunachukua mikopo tunadaiwa marejesho tutalipaje iwapo tutakimbizana na biashara kila siku, tunamwaga au kugawa bidhaa zinapobaki, tuna maisha ya digidigi.”

Katika mafunzo hayo yaliyotolewa na jukwaa hilo kwa kushirikiana na Chama Cha Wanasheria Wanawake nchini (Tawla), walitoa elimu kwa wanawake ili kuwajengea uwezo na kuwaelimisha juu ya kupinga ukatili wa kijinsia, ambao kwa kiasi kikubwa umekithiri katika eneo hilo.

 Awali baadhi ya wanawake walipinga vikali madai ya kwamba wanawake wengi wa eneo hilo ni walevi hali inayochangia kukithiri kwa matukio hayo.

Mmoja wa wanawake hao, Neema Adam, anasema zamani walikuwa wakiishi kwa amani ila tangu matukio hayo yaanze wamekuwa wakiishi kwa hofu na wengi wao hususani wafanyabiashara hulazimika kufunga biashara zao mapema wakihofia kufanyiwa vitendo hivyo vya kikatili.

“Tusidanganyane,  nakataa wanaodai wanawake wa hapa ni walevi, kwani kuna wengine wamefanyiwa vitendo hivyo na walikuwa hawanywi pombe na hata kama mtu anakunywa pombe ni sheria gani inayosema mlevi hana haki ya kuishi, na kama ulevi ingekuwa sababu mbona wanaume hawabakwi? anahoji na kuongeza:

“Inasikitisha kwani wengine waliokumbwa na ukatili huo wanakutwa wamewekewa nguo sehemu za siri, hatuelewi ni nini wanatoa huko, nawasihi akina mama tuache vyombo vya dola vifanye kazi yake ila tunaviomba vitoe majibu, wahusika wakamatwe na hatua za kisheria dhidi yao zichukuliwe,”

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la wanawake wilayani hapa, Biliuda Kisaka, anasema katika miaka ya hivi karibuni kumetokea mauaji ya wanawake wengi katika eneo hilo ila hadi sasa hawajaona ufumbuzi wa tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kukamatwa kwa wahusika na hatua za kisheria dhidi yao kuchukuliwa.

“Kupitia jukwaa hili tunajitahidi kuwaelimisha wanawake namna ya kujiamini, kutafuta haki zao na masuala mengine ya maendeleo ikiwamo kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, pamoja na kutoa taarifa ya matukio hao, haya yanayoendelea Mto wa Mbu yanatufedhehesha, hili tatizo linahitaji ufumbuzi wa haraka,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles