Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
JUMLA ya mitaala 79 ya shahada ya uzamili imepitiwa upya, huku 22 ikianzishwa katika shahada za awali na uzamili kupitia mradi wa HEET.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Kenneth Hosea wakati akifungua mkutano wadau mbalimbali ambao utudumu kwa siku mbili leo Novemba 6,2023 jijini Dar es Salaam.
Wadau hao wamekutana kujadili na kutoa mapendekezo ya kuboresha mapitio ya mitaala ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na kutoa maoni ya uanzishwaji wa kampasi ya chuo hicho mkoani Kigoma.
Dk. Hosea amesema anatambua kuwa kama nchi wana changamoto na uhaba mkubwa ya rasilimali watu wenye ujuzi na ubora kwenye sekta ya afya.
Amesema lengo mojawapo la mradi wa HEET hapo MUHAS ni kupitia upya mitaala ya uzamili na kubuni mipya kulingana na mahitaji ya nchi.
‘Jumla ya mitaala 16 ya shahada za uzamili imeanzishwa ambapo mitaala mitatu imeshapata ithibati kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) na inaanza kutumika mwaka huu na mitaala ya 13 itajadiliwa kwenye mkutano huu,”ameeleza.
Amesema mabadiliko ya elimu ya juu yanayolenga taasisi maalum kama MUHAS yanahitaji ushirikiano mpana na makini wa wadau ili kuhakikisha kwa mapitio ya mitaala yanashughulikia changamoto kubwa za rasilimali watu.
Amesema shughuli hizo mbili zipo ndani ya maeneo nane ya mradi wa elimu ya juu kwa mabadiliko ya uchumi (HEET) ambao ni mageuzi ya elimu ya juu kwa maendeleo ya uchumi hususani katika sekta ya afya.
” Siku hii ni muhimu yenye maan kubwa kufungua mkutano huu muhimu wa wadau ili kujadili mapitio ya mitaala katika jitihada za kuleta mabadiliko ya elimu yetu ya juu kwaajili ya kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini, “amesema Dk. Hosea.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Apolinary Kamuhabwa, amesema mwaka huu wanaadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa chuo hicho wakiwa na lengo la kuongeza idadi ya watumishi wa afya.
“Ushiriki wa wadau ni sehemu muhimu ya mitaala ya elimu ya juu, kwa ushiriki huu tunahakikisha matokeo ya mafunzo na ujuzi ambao wanafunzi wamepata unawiana na mahitaji ya sasa na ya baadaye ya waajiri na jamii,” amesema Profesa Kamuhabwa.
Aidha amesema kwa kuhusisha wadau hawa katika mapitio ya mitaala taasisi za elimu ya juu zinaweza kuongeza umuhimu na ushawishi program zao na kutayarisha wahitimu wao kwa changamoto na fursa za karne ya 21 mbeleni.
Naye Naibu wa Mradi wa HEET MUHAS, Dk. Nathanael Sirili, amesema kupata maoni ya wadau ni muhimu hivyo ujenzi wa kampasi ya Ujiji mkoni Kigoma unatarajia kuanza mwakani na utachukua muda wa miezi 24 hadi kukamilka.