NA RAMADHAN LIBENANGA – KILOSA
MIMBA za utotoni 4,186 sawa na asilimia 30 ya wajawazito waliohudhuria kliniki, zimeripotiwa wilayani Kilosa mkoani Morogoro kwa kipindi cha mwaka jana.
Mbali ya hiyo, kesi za wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na ujazito zimeripotiwa kuwa 15.
Akizungumza na MTANZA NIA ofisini kwake jana, Meneja Kanda wa Shirika la World Vision, Faraja Kulanga, alisema wameibaini tatizo hilo kutokana na kukusanya takwimu za maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Kulanga alisema kampeni ya kutokomeza ukatili dhidi ya watoto, hasa mimba na ndoa za utotoni, itasaidia kuwafanya watoto wa kike kufikia malengo yao ya maisha.
Alisema shirika hilo kwa kuona ukubwa wa tatizo, liliamua kupita na kuchunguza chanzo cha wingi wa watoto kupata mimba, jambo ambalo linapaswa kupata ufumbuzi wa haraka.
Kulanga alisema kesi za mimba zilizoripotiwa kwa shule za sekondari ni nane, saba zikiripotiwa kwa shule za msingi.
Naye Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Kilosa, Tumaini Mohammed, alisema kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, Shirika la World Vision limekuja na mradi wa kupiga vita ukatili kwa watoto wadogo.
Aliwaomba wananchi wilayani humo kushirikiana na Serikali kutoa taarifa kwa vyombo vya dola juu ya wazazi au mzazi anayeozesha mtoto aliye chini ya miaka 18.
“Msikae kimya kuona mtoto wa jirani yako amepewa mimba, wakati unajua anasoma, lete taarifa tufanye kazi sheria ifuate mkondo wake,” alisena Tumaini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mgoyi, alisema kampeni hiyo imekuja wakati mwafaka, hivyo kuwataka viongozi wa ngazi ya vijiji, kata hadi wilaya kushirikiana na shirika hilo.