Na Derick Milton, Simiyu
Mkuu wa Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, Gabriel Zacharia amesema matukio ya wanafunzi wa kike kupewa mimba wilayani humo yanaongezeka kwa kasi kubwa jambo ambalo limeendelea kumsumbua akili yake.
Zacharia amesema hayo Mei 24, 2022 katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichofanyika Nyashimo.
Amesema kila mwezi kwenye kikao cha kamati ya ulinzi na usalama Wilaya matukio ya Mimba za wanafunzi yanaongoza kuripotiwa kwenye kikao hicho kila mwezi.
“Matukio mengi ambayo tumekuwa tukikutana nayo kwenye kamati ya ulinzi na usalama wa Wilaya kila mwezi, mengi ni mimba kwa wanafunzi, tatizo hili limekuwa kubwa sana, kila tunapokaa kikao matukio mengi yanayokuwepo ni mimba za wanafunzi.
“Tatizo hili ni moja kati ya vitu ambavyo leo ukiniuliza…kitu gani kinachokusumbua akili…nasumbuliwa na mimba, nasumbuliwa na mambo ya mimba kwa wanafunzi katika wilaya hii,” amesema Zacharia.
Kwenye kikao hicho Mkuu huyo wa Wilaya amewataka madiwani kushirikiana na Serikali katika kupambana na tatizo hilo, ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wananchi kuacha kuharibu ushahidi pindi wahusika wanapofikishwa mahakamani.
“Na kinachofanya mambo haya yawe magumu ni huu utaratibu ambao wahusika humalizana kifamilia, hivyo kusababisha mwanafunzi aliyepewa mimba kuharibu ushahidi, tusaidiane kupambana na tatizo hili,” amesema Zacharia.