29.9 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Mikoa mitano yaunganishwa na gesi asilia

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM

NAIBU Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema Serikali imekamilisha mpango wa awali wa kusambaza gesi asili kwenye mikoa mitano nchini.

Mgalu alisema usambazaji huo unafanyika ili kuhakikisha Tanzania inatumia rasilimali hiyo kuelekea uchumi wa kati wa viwanda.

Alisema kabla ya kukamilisha mpango huo, kulifanyika utafiti wa miaka mitatu uliofanywa na Serikali kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (Jaica).

Alitaja mikoa iliyounganishiwa nishati hiyo kuwa ni Arusha, Dodoma, Tanga, Kilimanjaro na Morogoro huku akibainisha kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha mikoa yote Tanzania inapata nishati hiyo kwa matumizi mbalimbali.

Mgalu alisema Tanzania imegundua gesi asilia yenye ujazo wa futi trilioni 57 ambayo inatengenezewa mkakati wa matumizi yake.

Alisema hadi sasa gesi asili inazalisha megawati 800 za umeme kati ya 1,601 zinazotarajiwa kuzalishwa kwa kutumia nishati hiyo.

Mgalu alisema gesi hiyo ya asili inatumika pia kwenye magari na hadi sasa magari 200 yanatumia gesi na miundombinu ya kuisambaza inaendelea.

Alisema gesi asili inasaidia pia kutunza mazingira, hasa kwenye kupikia na hadi sasa Shirika la Maendeleo la Petroli (TPDC), limesambaza miundombinu ya gesi ya kupikia majumbani mikoa ya Lindi, Mtwara, Dar es Salaam na Pwani.

Mgalu pia alisema kuhusu matumizi ya gesi viwandani, hadi sasa viwanda zaidi ya 50 vimeunganishwa.

Naye Kamishna wa Maendeleo ya Petroli na Gesi, Adam Zuberi, alisema Tanzania ipo kwenye wakati sahihi, hivyo jitihada za makusudi zinafanyika kufikisha gesi asili mikoa yote Tanzania.

Naye Mshauri wa Taasisi ya Nishati na Uchumi wa Japan, Kensuke Kanekinyo, alisema awamu ya kwanza ya mradi huo imetumia Dola za Marekani milioni mbili ndani ya  miaka mitatu.

Alisema gharama za mradi wote ni dola milioni 250 zitakazotumika kupeleka gesi mikoa yote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles