Na JOHANES RESPICHIUS
UTAMU kolea! Soko la filamu nchini linaendeleza juhudi za kujitanua kimataifa baada ya mwigizaji kutoka Nigeria, Mike Ezuruonye kutua nchini kwa ajili ya kucheza sinema na wasanii wa Bongo Muvi.
Ujio wake ni mwaliko kutoka kwa staa wa filamu Bongo, Halima Yahaya a.k.a Davina ambaye alichipushwa na Kundi la Sanaa la Kaole la jijini Dar es Salaam takribani muongo mmoja uliopita.
Historia ya Davina ni ndefu, amefanya sinema nyingi kwa ustadi mkubwa kama ilivyo kwa Mike ambaye mbali na kushiriki sinema nyingi za Nollywood lakini pia ameshiriki na kushinda tuzo mbalimbali nchini Nigeria.
Kama ni kwenye sherehe tunaweza kusema ndiyo kwanza mshereheshaji anajaribu kipaza sauti ili kuona ikiwa kinafanya kazi vizuri kama wasikikavyo wakisema: “One, two… one two test, tunajaribu!”
Muda wowote Mike, Davina na crew nzima iliyoandaliwa na Davina mwenyewe kupitia Kampuni ya Project and Design ambayo yeye ni mkurugenzi, wataingia location kwa ajili ya kuanza kazi ya kurekodi sinema ambayo mpaka sasa haijajulikana jina.
Ushiriki wake katika ulingo wa filamu za Kibongo ni chachu ya mafanikio kwa wasanii wetu na soko la Bongo Muvi kwa ujumla.
Ni mwendelezo wa juhudi zilizofanywa awali na marehemu Steven Kanumba, wakati akifanya kazi na Kampuni ya Game 1st Quality na baadaye kwenye kampuni yake binafsi ya Kanumba The Great Film.
Sinema ya kwanza ya Kanumba kucheza na mastaa wa Nigeria mwaka 2007 ilikuwa ni Dar 2 Lagos, kabla ya kuendeleza moto huo kwenye Cross My Sin, The Director na nyinginezo.
Akiwa na Kanumba The Great alifanikiwa kumleta msanii bei mbaya Nollywood, Ramsey Noah na kucheza naye sinema ya Devil Kingdom ambayo ndani yake wamo mastaa kibao wa Bongo wakiwemo Kajala Masanja, Senator Msungu na wengine.
Mike, amefanya kazi nyingi na kumpa heshima kubwa Nollywood zikiwemo Broken Marriage, God Bless Me, Return of Tattoo na Critical Decision zilizompaisha na kumuweka pazuri katika sinema za Nollywood. Ujio wake nchini unaweza kuwa na tija kwa afya ya filamu za Kibongo ikiwa watafanya kazi yenye ubora na kuzingatia viwango.
Akizungumzia ujio wa staa huyo wa Nigeria, Davina anasema ushirikiano alioupata kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliyo chini ya Waziri Nape Nnauye ulimrahisishia ujio wa mkali huyo.
“Atakuwa hapa Tanzania kwa wiki mbili, naamini ujio wake utafungua soko la kimataifa na hasa Nigeria,” anasema Davina.
WAZIRI NAPE
Katika mapokezi ya msanii huyo Jumatatu wiki hii katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, ambayo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alihudhuria, katika hotuba yake alisema:
“Huyu ni miongoni mwa wasanii waliokuja na watakaoendelea kuja nchini na kama Serikali tutaendelea kutengeneza mazingira mazuri ili waje wengi zaidi washirikiane na sisi kwani wanaleta teknolojia, ujuzi na uzoefu wao.
“Kama wakishirikiana kufanya kazi na wasanii wetu, kazi zetu zitapata soko katika nchi yao na sote kwa pamoja tutafaidika,” anasema Nape.
Akaongeza kuwa, umefika wakati wa wasanii wa Tanzania kutumia filamu na muziki kuiunganisha Afrika hivyo ni jukumu la wasanii kufanya kazi kwa bidii ili bara letu lijivunie kuwa nao popote pale ulimwenguni.
MIKE KWA UFUPI
Mike alizaliwa Septemba 21, 1982 jijini Lagos, Nigeria. Ni mhitimu wa Shahada ya Uhasibu kutoka Chuo Kikuu cha Nnamdi Azikiwe.
Alifunga ndoa ya kimila Mei, 2010 na mkewe Nkechi Nnorom, kabla ya kufunga ndoa ya kanisani, Jumamosi ya Mei 13,2010 huko Lagos.