NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
SERIKALI imeainisha mikakati saba itakayotekelezwa katika kipindi cha muda wa kati ili kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa lengo la kuiwezesha kugharamia shughuli zake.
Akizungumza jana wakati wa kuwasilisha bajeti ya mwaka 2019/2020, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema wameandaa mikakati mahsusi ya kiutawala ili kufikia malengo ya makadirio ya mapato ya ndani.
Mikakati hiyo inajumuisha kutekeleza Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Mapato ya Ndani (Integrated Domestic Revenue Admistrative System – IDRAS) na kupanua wigo wa kodi kupitia utambuzi na usajili wa walipakodi wapya pamoja na kuendelea na urasimishaji wa sekta isiyo rasmi.
Mingine ni kuwekeza katika maeneo ambayo Serikali inaweza kupata mapato zaidi, hususan katika uvuvi wa bahari kuu kwa kujenga bandari ya uvuvi na ununuzi wa meli za uvuvi.
“Tunakusudia kuimarisha uwezo wa ufuatiliaji na udhibiti wa uhamishaji wa faida unaofanywa na kampuni za kimataifa na kuimarisha usimamizi wa misamaha ya kodi kwa kuhakikisha inaelekezwa kwenye miradi inayokusudiwa,” alisema Dk. Mpango.
Kwa mujibu wa Waziri Mpango, mikakati mingine ni kuhakikisha kuwa maduhuli yote yanapitia katika Mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato (GePG) na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji katika taasisi za Serikali ili kuhakikisha michango stahiki ya taasisi za umma kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali inawasilishwa kwa wakati.
Alifafanua katika kufanikisha lengo hilo, Serikali itatekeleza sera mbalimbali ili kupanua wigo wa kodi na mapato mengine ya Serikali.
Sera hizo ni kuboresha mazingira ya kufanya biashara ili kuvutia uwekezaji, ukuaji wa biashara ndogo na za kati, kurekebisha viwango vya kodi kwa lengo la kuhamasisha uzalishaji na kulinda viwanda vya ndani dhidi ya ushindani kutoka nje.
“Kuboresha mazingira ya ulipaji kodi kwa hiyari, upanuzi wa wigo wa kodi na matumizi ya tehama katika usimamizi wa kodi,” alisema Dk. Mpango.
Sera nyingine alisema ni kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato, pamoja na kuweka mkazo zaidi katika kutoa elimu kwa mlipakodi na kuimarisha makusanyo yasiyo ya kodi kwa kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya tehama.
Dk. Mpango alisema wataendelea kuwianisha na kupunguza tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na wakala, taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuiongezea Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).