Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
MIILI ya askari 14 wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), waliouawa mwishoni mwa wiki Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), itarejeshwa nchini kati ya Desemba 12 au 13 mwaka huu.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaama jana na Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali, James Mwakibolwa alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema Serikali inashirikiana na Umoja wa Mataifa (UN) kuhakikisha miili ya askari hao inarejeshwa nchini.
“Miili ya askari 14 waliouawa DRC itarejeshwa nchini kati ya Jumanne Desemba 12, au Jumatano Desemba 13, mwaka huu,” alisema Mwakibolwa.
Akizungumzia kuuawa kwa askari hao, Mwakibolwa alisema walivamiwa kambini na waasi wa ADF na mapigano yalidumu kwa saa 13.
Alisema askari 14 wa JWTZ waliuawa, 44 walijeruhiwa na wengine wawili hawajulikani walipo.
Jenerali Mwakibolwa alisema tukio hilo lililotokea Desemba 7 mwaka huu katika kambi ndogo iliyopo katika Daraja la Mto Simulike, Kaskazini Mashariki mwa Wilaya ya Beni, Jimbo la Kivu.
Alisema shambulio hilo ni kubwa zaidi kutokea tangu JWTZ ianze kushiriki ulinzi wa amani DRC mwaka 2011.
“Hivi sasa taratibu za kusafirisha miili ya marehemu kuirejesha nchini inafanyika chini ya uratibu wa Serikali na Umoja wa Mataifa.
“JWTZ na Serikali tunaendelea kuchukua hatua stahiki kufuatilia tukio hili ikiwamo kufanya uchunguzi katika eneo husika,”alisema.
Mnadhimu huyo Mkuu wa JWTZ alisema tukio hilo halitawavunja moyo JWTZ wala kutetereka kupeperusha bendera ya Tanzania ndani na nje ya nchi bali linawaongezea ari, nguvu, ushupavu na uhodari katika kutekeleza majukumu yao.
“Ni bahati mbaya mashujaa wetu wameuawa wakiwa wanatekeleza jukumu la ulinzi wa amani DRC. Kwa umoja wetu Watanzania tuwaombee dua roho zao zipumzike kwa amani na majeruhi wapone haraka iwezekanavyo warejee kutekeleza majukumu yao,” alisema.
Katika kipindi cha miezi sita tukio hilo la kuuawa askari wa JWTZ ni la pili kutokea baada ya Oktoba, mwaka huu wanajeshi wawili wa waliokuwa katika kundi la walinda amani kuuawa na wengine 18 kujeruhiwa.