Mohamed Hamad, Kiteto
Mkuu wa Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, Mhandisi Tumain Magesa amesema uanzishwaji wa nyanda za malisho wilayani humo ni kutaka kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji na ndio maana zinakuwa chini ya kijiji husika.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Dosidosi Januari 10 mwaka huu, alipokuwa akiwatolea ufafanuzi juu ya uanzishwaji huyo DC Magesa alisema kuna bà adhi ya wananchi wanapotosha umma juu nyanda hizo.
“Kimsingi kinachofanyika ni Wizara ya Mifugo kutaka kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kuja na mkakati uliopo kwenye Ilani ya CCM na kuutekeleza kwa kutengeneza nyanda hizo, ” alisema.
Alisema nyanda za malisho zinaanzia kijijini kwa wananchi wenyewe kujadiliana na kufikia muafaka, uelewa wa wananchi umekuwa ukisumbuliwa na baadhi ya watu wakisema kuwa hifadhi zimeongezeka sana wengine nyanda za malisho na kuwataka wawe makini.
Aidha Magesa alizitaja nyanda hizo kuwa ni Olengapa na Alole zilizopo tarafa ya Kijungu na Napalay iliyopo Kata ya Partimbo ambapo alidai kuwa zipo katika hatua za ukamilishwaji.