Na UPENDO MOSHA- MOSHI
OFISI za Bonde la Mto Pangani, mkoani Kilimanjaro, imekiri kuwapo kwa ongezeko kubwa la migogoro kati ya wakulima na wananchi wa kawaida inayosababishwa na uhaba wa maji.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisa wa Bonde hilo, Mtoi Kanyawana, alisema migogoro ya maji imekuwa ikiongezeka siku hadi siku kutokana na ukame kuyakumba baadhi ya maeneo nchini.
“Hadi sasa tumepokea malalamiko kutoka maeneo mbalimbali ikiwamo katika vijiji 19 vya Wilaya ya Moshi, mkoani hapa vyenye wakazi zaidi ya 56,000.
“Wananchi hao wanadai kukosa huduma ya maji ya kunywa na matumizi ya nyumbani kutokana na uwepo wa mradi wa kilimo cha umwagiliaji wa Kirua Kahe.
“Changamoto kubwa inayosababisha vyanzo vingi vya maji kuvamiwa na kuharibiwa vibaya na wananchi ni kutokana na kubadilika badilika kwa uongozi wa maeneo ya vijiji, hali ambayo inasababisha mfumo wa matumzi ya maji kubadilika.
“Hata hivyo, kwa sasa tupo katika mchakato wa kuainisha na kuyapandisha hadhi baadhi ya maeneo ya vyanzo vya maji na kuyahifadhi ili kuhakikisha vyanzo hivyo vinalindwa na tatizo la upungufu wa maji linakwisha,” alisema Kanyawana.
Kwa mujibu wa Kanyawana, maeneo yote ambayo yanategemewa kupandishwa hadhi na kuwa hifadhi, yatakuwa chini ya miliki ya bonde hilo na jukumu la kusimamia maeneo hayo wataliacha kwa Serikali za mitaa na vijiji kwa kushirikiana na jumuiya za watumia maji.
“Yapo maeneo ambayo ni vyanzo vya maji, tuna mpango wa kuja kuyatangaza ili yajulikane rasmi ili wananchi ikiwamo wafugaji ambao wataingia, waweze kuwajibishwa kisheria.
“Lakini pia, maeneo mengine ambayo yana vyanzo vya maji husimamiwa na jumuiya za watumia maji ambazo zipo kisheria,” alisema.
Pamoja na hayo, alisema suala la utunzaji wa mazingira katika vyanzo vya maji ni jambo muhimu na si jukumu la ofisi za Bonde la Mto Pangani peke yake.