JERRY MURO AKUBALI YAISHE

Jerry Muro
Jerry Muro
Jerry Muro

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya soka ya Yanga, Jerry Muro, ameliandikia barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuomba kupunguziwa adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja baada ya kutumikia nusu ya kifungo hicho.

Kamati ya Maadili ya TFF, Julai mwaka jana ilimfungia Muro kutojihusisha na masuala ya soka pamoja na kumtoza faini ya shilingi milioni 3 baada ya kumkuta na hatia katika mashtaka mawili kati ya matatu, yaliyowasilishwa na TFF mbele ya Kamati hiyo iliyokuwa chini ya Wakili Wilson Ogunde.

Makosa yaliyomtia hatiani Muro ni kudharau maamuzi ya Kamati ya Nidhamu ya TFF mwaka 2015, alipotakiwa kulipa faini ya Sh milioni 5 baada ya kufanya makosa.

Shtaka lingine ni kuchochea vurugu na kuhatarisha amani kuelekea mchezo wa Kundi A wa Kombe la Shirikisho kati ya Yanga na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo timu yake ilifungwa bao 1-0.

Kutokuwepo kwa Ofisa habari huyo mwenye maneno ya kinazi yaliyokua yanatia hamasa hasa pale alipojibizana na Ofisa mwenzake wa habari wa klabu ya Simba, Haji Manara, kumepoteza ladha na hamasa katika soka hali iliyomfanya swahiba wake huyo kuwa wa kwanza kuandika barua kwa TFF kumwombea msamaha na kumwondolea kifungo.

Lakini pia kutokuwepo kwa Muro, kumeathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa taarifa kutoka katika klabu ya Yanga, kwani licha ya mambo ya kibinadamu ya Muro alikuwa ni kati ya maofisa habari bora wanaokidhi haja za wapokeaji taarifa hizo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Muro alisema barua hiyo aliwasilisha TFF Januari mbili mwaka huu, akieleza kuwa ni baada ya kushawishiwa na mashabiki na wadau wa soka baada ya kuona anahitajika kuongeza hamasa katika mchezo huo nchini.

“Nimeandika barua kwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi kwa kuwa yeye ndiye mwenye dhamana kubwa na ambaye anaweza kutengua adhabu yangu kulingana na mamlaka aliyonayo katika shirikisho hilo.

“Nimefanya hivyo baada ya mchezo wa soka kukosa hamasa kwa kipindi kirefu tangu nifungiwe na Kamati ya Maadili, mbali na swahiba wangu Haji Manara kuniombea msamaha, wadau, mashabiki na waandishi wa habari wameniomba pia kufanya hivyo ili niweze kutoka katika kifungo,” alisema Muro.

Muro alisema kuwa ameandika barua hiyo pia ili arudi aweze kushirikiana na wadau wengine wa soka, katika kulisukuma gurudumu la mpira wa miguu nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here