26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mifuko 800 ya sukari yakamatwa

sukari*Ilikuwa ikiandaliwa kufichwaa kwenye maghala

*DC asimamia ugawaji Arusha, aoonya watendaji

 

Na Peter Fabian, Mwanza

MAPAMBANO  kati ya vyombo vya dola na wafanyabiashara wanaodaiwa kuficha sukari  yameendelea maeneo mbalimbali nchini huku mifuko ya bidhaa hiyo ikikamatwa mkoani Mwanza.

Taarifa kutoka mkoani Mwanza  zinasema Kikosi cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa  huo, kimekamata mifuko 800 kati ya 1,200 ya kilo 50  ambayo  ilikuwa ikishushwa kwenye ghala la mfanyabiashara mmoja kwa ajili ya kufichwa.

Sukari hiyo  ilikamatwa juzi   jioni katika Mtaa wa Rufiji, Mwanza ikiwa kwenye gari   ya Scania  namba    T 200 BSV  na tela lake   namba   T 601 DFM, ikiwa limeegesha katika ghala la Adam Michael Balenga.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Augustine Senga alisema baada ya kukamatwa sukari hiyo  mhusika  alidai ilikuwa imetoka Kampuni ya Al Naem Enterprise Ltd ya  Tabata, Dar es Dar es Salaam.

“Tumekamata sukari mifuko 800 ya kilo 50. Hii ilikuwa ikiuzwa kwa siri nyumbani kwa mfanyabiashara… wakati tunakamata tayari kiasi kingine cha mifuko 400 ilikuwa imekwisha kuuzwa,” alisema Senga.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema kikosi kazi kimeanza kazi vizuri na   bado kinafuatilia nyendo za baadhi ya wafanyabiashara ambao wanaonekana kuanza kutoa sukari na kuiuza kwa siri baada ya agizo la Rais Dk. John  Magufuli.

“Tumepata taarifa kuna sukari kutoka Kagera imeingizwa kupitia Ziwa Victoria.  Tunataka kujua ni sukari ya Kagera kweli au ya Kenya na Uganda, wapo ambao walikuwa wameficha kwenye maghala yao sasa kutokana kauli ya rais ameanza kuitoa kuingiza sokoni na wanaendelea kuuza kwa bei juu,” alisema.

Kukamatwa kwa shehena hiyo  ni mwendelezo wa agizo la Rais Magufuli   juzi akiwa mkoani Arusha la  kuwataka wafanyabiashara walioficha bidhaa hiyo kuitoa na kuisambaza kwa ajili ya kuiuza kwa wananchi.

Alisema  iwapo watakiuka, itataifishwa kwa nguvu na kugawiwa bure kwa wananchi.

 

ARUSHA

Taarifa kutoka mkoani Arusha  zinasema baada ya jeshi la polisi kumkamata  na kumhoji mfanyabiashara wa sukari, Abdul Karim Dakik kwa tuhuma za kuficha bidhaa hiyo, imebainika sukari iliyokuwa kwenye ghala lake ilihifadhiwa kwa maelekezo ya Serikali.

Kutokana na uhaba wa sukari, tayari tani 42 za sukari hiyo zimeanza  kugawanywa katika kata zote za Jiji la Arusha kwa usimamizi wa viongozi wa Serikali ngazi zote za wilaya.

Hata hivyo, kinyume na agizo la Rais John Magufuli kuwa sukari itakayokamatwa katika ghala igawanywe bure kwa wananchi, hali ilikuwa tofauti kwa vile  sukari iliyokamatwa katika ghala la Kampuni ya Alpha Group iliuzwa kwa bei elekezi ya Serikali ya Sh 1,800.

Akizungumza na maofisa  watendaji wa kata zote 25 za jiji hilo jana kabla ya kugawa sukari hiyo,  Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Fadhili Nkurlu alionekana  kufadhaishwa na tukio la kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo.

“Ni bahati mbaya sana ndugu yetu Dakik aliingia na kukumbana na msukosuko siku ya jana (juzi) bila sababu akidhaniwa ameficha sukari.

“Tayari alishatuletea taarifa ya sukari aliyokuwa nayo,  naomba tusahau yaliyopita yalikuwa maagizo ya Rais,” alisema Nkurlu mbele ya watendaji hao.

Kabla ya kuchukua hatua hiyo aliitisha kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kuangalia namna bora ya kugawa sukari hiyo.

Aliwatahadharisha na kuwaonya watendaji hao  kusimamia wafanyabiashara katika maeneo yao  ili wauze sukari kwa bei elekezi na si vinginevyo.

Katika ugawaji huo ambao umeitwa awamu ya majaribio, baadhi ya kata zilipewa kilo 600  nyingine 1,000 huku kata zenye idadi kubwa ya wakazi zikipewa kilo 1,700, ambazo zilikabidhiwa kwa watendaji hao.

“Tunaigawa sukari hii kama hatua ya  awali, tutagawa tena hadi  tutakapomaliza tani  42 zilizopo… mkasimamie vizuri kila kaya isinunue zaidi ya kilo moja na kwa bei elekezi,” alisisitiza Nkurlu.

Alisema atakuwa akizunguka mchana na usiku katika mitaa yote ndani ya wilaya   kujionea mwenyewe iwapo maagizo hayo ya Serikali yanafuatwa.

Aliwakemea baadhi ya wafanyabiashara wanaokaidi maelekezo ya Serikali kuhusu bei za bidhaa mbalimbali na kuwataka kuacha mara moja.

“Kamati ya ulinzi na usalama iko kazini, tunapita katika mitaa na maduka yote.  Tutakapobaini sukari inauzwa bei tofauti tutachukua hatua kali za  sheria  ikiwamo kuwafutia leseni wafanyabiashara watakaobainika,” alisema Nkurlu.

Wakizungumzia ugawaji wa sukari kilo moja kwa kila kaya, baadhi ya maofisa watendaji wa kata walisema itakuwa na changamoto na lawama nyingi kwa kuwa sukari ni bidhaa inayotumika kila siku na ni vigumu kumudu changamoto zake.

“Tutafanikiwa endapo wote tutashirikiana, lakini kwa mfano kata yangu ndiyo kituo kikuu cha biashara, soko kuu lipo, kituo kikuu cha mabasi na maduka yote makubwa… haya yote yanavuta watu kutoka nje ya kata huoni ni vigumu kuwadhibiti ili wanunue kilo moja tu kwa kaya?” alihoji   Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kati, Suleiman Kinyigo.

Vilevile, hali ni tofauti katika mitaa mbalimbali ambako  bado sukari  inauzwa Sh 2,800 na Sh 3,500 kwa kilo moja, huku wateja wakilazimika kupanga msururu   wapate angalau kidogo.

Katika maduka makubwa (super market), wauzaji walidaiwa kuelekezwa na wamiliki wa maduka hayo kutouza zaidi ya kilo mbili kwa mteja moja ili watu wasitumie upungufu wa bidhaa hiyo kujilimbikizia na kuacha wengine wakikosa.

“Binafsi katika duka langu nauza sukari kwa bei ya Sh 2000 kwa kilo, lakini  nimewaelekeza wauzaji wasiuze zaidi ya kilo mbili kwa mteja moja, na tumepima kwa ujazo wa kilo moja moja.

“Lengo letu ni kudhibiti watu wenye tamaa ambao wangependa kununua kwa wingi,” alisema Anselm Minja, mmiliki wa Clock Tower Super Market.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles