Na Walter Mguluchuma-Katavi
MAHAKAMA ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imemuhukamu  kwende jela miaka 30, mkazi wa Mtaa wa Majengo, Ramadhani Shaban ( 24), baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka kiziwi ambaye ni mgonjwa wa afya ya akili.
Hukumu hiyo iliyovuta hisia za watu wengi wa Manispa ya Mpanda, ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Gosper  Luoga, baada ya mshtakiwa kusomewa mashtaka na kukiri kutenda kosa hilo la kumbaka kiziwi huyo.
Awali mwendesha Mashtaka wa Serikali, Flaviana Shio,  alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa Ramadhani  Shabani, alitenda kosa hilo Septemba 9, mwaka huu saa 12 jioni katika Mtaa wa Majengo B.
Ilidaiwa mahakamani hapo kwamba siku hiyo ya tukio mshtakiwa alikwenda katika Mtaa wa Mji Mwema alikokuwa akiishi kiziwi huyo kwa mjomba wake aliyetajwa kwa jina la Ernest Chambala na kumpakia kwenye baiskeli yake na kuondoka naye.
Mshtakiwa huyo baada ya kumpakia kiziwi huyo alikwenda naye hadi kwenye chumba chake alichokuwa amepanga Mtaa wa Majengo B na kisha alianza kumbaka hadi alipomaliza haja yake.
Mwendesha mashtaha huyo aliendelea kuiambia mahakama kwamba baada ya kiziwi huyo kubakwa alitoka nje na kuanza kuwaonyesha watu ishara iliyokuwa ikionyesha amebakwa.
Mjomba wa kiziwi huyo, Ernest Chambala alianza kumsaka mtu aliyetenda unyama huo, ambapo alimwongoza hadi kwenye nyumba aliyokuwa amepanga Ramadhani na kumwonesha chumba cha kijana huyo.
Kutokana na hali hiyo mjombe huyo aliwauliza majirani kama walimwona binti huyo akiingia ndani ya chumba cha mshtakiwa huyo, ambapo walithibisha kumwona akiingia kwenye chumba cha kijana huyo.
Baada ya muda mshtakiwa alikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Mpanda  ambapo katika maelezo yake alikiri kumbaka kiziwi huyo na alipopimwa ilionekana katika sehemu zake za siri kuna mbegu za kiume.
Baada ya maelezo hayo Hakimu Luoga, alisema kwamba mahakama imemtia hatiani mshtakiwa huyona kumpa nafasi ya kujitetea.
Katika utetezi wake mshtakiwa huyo aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa mama yake anamtegemea kwani baba yake mzazi alishafariki dunia.
Pamoja na utetezi huo, Hakimu Luoga alisema mahakama imemtia hatiani kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 130 (1) (2) e na kifungu namba 131 (1) cha Sheria ya Kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002 kwa kumuhukumu kifungo cha miaka 30 jela.
Hakimu Luoga, alisema katika hukumu hiyo mahakama pia imezingatia hali ya ongezeko la matukio ya mara kwa mara ya ubakaji.