NA LEAH MWAINYEKULE,
WIKI iliyopita nilimsikiliza Rais John Magufuli akizungumza na watani zake wa Dar es Salaam. Aliwaambia kwamba kutokana na juhudi za Serikali yake kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, basi hawana budi kuupa likizo uzazi wa mpango na kuendelea kufyatua watoto.
Aliyasema hayo huku akicheka. Inawezekana alikuwa akicheka kutokana na ukweli kwamba alikuwa akiongea na watani zake au inawezekana alikuwa akicheka kwa kuwa hakumaanisha sana hilo alilolisema la kuweka kando uzazi wa mpango.
Ukweli ni kwamba, hata lugha aliyoitumia ya ‘kufyatua’ ilikuwa ya masihara, kwani wengi tumezoea lugha hiyo ikitumika kwenye matofali.
Sina hakika kama Rais alikuwa akifanya matani au alimaanisha. Nilicho na uhahika nacho ni hili la utoaji wa elimu bure ambayo ni kweli Serikali yake imedhamiria kulisimamia. Vile vile, sina uhakika kama utoaji wa elimu bure ndiyo unapaswa kufanywa kuwa tiketi ya watu ‘kufyatua’ watoto kama matofali.
Nilitazame kwa pande mbili. Upande wa kwanza ni wa matani ya rais kwa watani zake wa Dar es Salaam. Pamoja na kuwa kweli kwamba Mheshimiwa na watu wa Dar es Salaam ni watani wa kikabila, bado yeye ni Amiri Jeshi, kwa maana ya kwamba neno analolitamka, liwe matani ama la, ni agizo.
Kutokana na neno la Rais kuwa agizo, basi watani zake wa Dar es Salaam wanaweza wakaamua ‘kufyatua’ kweli watoto, huku wakiwa na imani kwamba watoto hao wakipata elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, basi maisha yamekuwa mazuri.
Wakati huo huo, wanaweza kusahau kwamba suala la malezi na makuzi ya mtoto si elimu peke yake, bali Serikali hii hii ya mtani wao Magufuli haitawapa chakula cha bure tena ameshatamka kwamba hatagawa chakula bure.
Wakasahau kwamba Serikali hii hii ya mtani wao Magufuli haitawapa mavazi ya bure, wala haitawajengea makazi ya bure. Hayo yote yatakuwa juu ya wazazi walioamua ‘kuwafyatua’ watoto, ili waweze kufaidi elimu ya bure.
Lakini nikilitazama kwa upande wa pili, najaribu kufikiri kwamba huenda Rais alimaanisha alichokisema. Kwamba masuala ya uzazi wa mpango kwake hayana faida sana na hata juhudi zilizokuwa zikifanywa na mashirika mbalimbali, yakiwemo ya Serikali, kuhamasisha uzazi wa mpango, zimefika ukomo.
Najaribu kufikiri kwamba kama hivyo ndivyo Rais anavyowaza na kwa kuwa neno lake ni agizo, basi hata zile juhudi za kusaidia kupunguza vifo vya akina mama mabao waliathirika kutokana na kuzaa kila mwaka, zimefika ukomo.
Nawaza kwamba kumbe hata juhudi za kupunguza lishe duni kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ambao wanakosa malezi stahiki kutokana na mama zao kutakiwa kuwahudumia zaidi wale wachanga waliotoka kuzaliwa, zimefika ukomo.
Ndiyo maana nalazimika kumwomba Rais kuirejea kauli yake, iwe ya matani ama la na badala ya kuwafundisha watani zake kufyatua watoto, basi awasaidie kuwalea wale watoto ambao tayari wapo. Hapa ninawazungumzia watoto wale ambao tayari wamezaliwa, lakini wanaishi katika mazingira hatarishi.
Nani asiyejua kwamba hapa Tanzania kuna watoto ambao wamefiwa na wazazi wao na ndugu waliotarajiwa kuwalea wameamua kuwafukuza kwenye nyumba za wazazi wao na kujirithisha wenyewe?
Nani asiyefahamu kwamba wapo watoto wengine maeneo mbalimbali ya nchi ambao wametelekezwa, wanajilea wenyewe na asubuhi wanapokwenda shuleni ambako wanasoma bure wanakwenda wakiwa na njaa, jioni wakirudi wanachemsha mahindi na kuyala ili waweze kuendelea kuishi?
Nani asiyeona kwamba wapo hata watoto wa Dar es Salaam kwa watani zake Rais ambao wamegeuka ombaomba, wakizunguka kutoka gari moja hadi lingine kwenye taa za barabarani, wakibembeleza wapewe chochote ili waweze kuendeleza maisha yao?
Rais, badala ya kuwashawishi watani zako wa Dar es Salaam kuendelea kufyatua watoto, unaonaje ukiwasaidia kuwalea wale ambao tayari wapo?