26.9 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Mgonjwa wa pili apona corona

 AVELINE KITOMARY Na BRIGHITER MASAKI -DAR ES SALAAM 

MGONJWA mmoja wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19) nchini amepona, huku mwingine akithibitika kuwa na virusi hivyo. 

Kutokana na taarifa iliyotolewa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, hadi sasa watu waliothibitika kuwa na virusi hivyo nchini ni 20 huku wawili wakiwa wamepona na mmoja kufariki dunia. 

Wakati hali ikiwa hivyo nchini, hadi jana waliofariki dunia kwa virusi hivyo duniani ni zaidi ya 42,000 huku 178,000 wakiwa wamepona na 860,000 wamethibitika kuwa na virusi hivyo. 

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Waziri Ummy jana, ilisema mmoja kati ya wagonjwa waliokuwa katika kituo cha matibabu cha Temeke, Dar es Salaam juzi amethibitika kupona. 

“Ameruhusiwa kurudi nyumbani na hivyo kufanya jumla ya watu waliopona kuwa wawili,” alisema Ummy. 

Machi 26, Ummy alitangaza kupona kwa mgonjwa wa kwanza, Isabela Mwampamba (46). 

Machi 16, Ummy alimtangaza Isabela kuwa mgonjwa wa kwanza wa corona ambaye aliwasili nchini akitokea Ubelgiji. 

Baada ya Isabela kugundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo, aliwekwa karantini na Serikali iliendelea kuwafuatilia watu wake wote wa karibu ili kubaini hali zao. 

MGONJWA MPYA 

Jana kwenye taarifa yake, Ummy alitangaza kubainika kwa mgonjwa mpya ambaye ni mwanamke mwenye umri wa miaka 42, raia wa Marekani. 

“Wizara inathibitisha kuwepo kwa kesi mpya ya maambukizi ya virusi vya corona (Covid-19) nchini iliyopatikana jijini Dar es Salaam, mgonjwa huyo amekuwa karibu na mtu aliyesafiri nje ya nchi na kuthibitika kuwa na maambukizi ya virusi vya Covid-19 aliporejea nchini. 

“Hivyo hadi sasa jumla ya kesi za maambukizi ya virusi vya corona (Covid-19) zilizothibitishwa hapa nchini ni 20. 

“Aidha ninatoa taarifa kuwa Machi 31 mwaka huu mmoja wa wagonjwa waliokuwa katika kiituo cha matibabu cha Temeke amethibitika kupona maambukizi aliyokuwa nayo na amerudishwa nyumbani,” alieleza Ummy. 

MAKONDA NA KODI 

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amewataka wamiliki wa nyumba za kupanga, maofisi, vibanda na hoteli kwenye mkoa wake kuwapunguzia wapangaji wao kodi kwa asilimia 50 katika miezi mitatu kutokana na hali ya uchumi wakati huu wa janga la corona. 

“Nimeongea na wenye nyumba na kuwataka wapunguze kodi kwa asilimia 50 ili kusaidia kufanya biashara na kuangalia hali ya uchumi ilivyo kwa sasa, kama mnavyofahamu corona imeathiri hali ya kifedha. 

“Tuwasaidie wenzetu waweze kupata fedha ya kununua chakula na kuweka ndani chakula kwa kuwapunguzia majukumu kama kodi za nyumba, fremu na hoteli,” alisema Makonda. 

Pia alitangaza kuwa madereva wa bodaboda na bajaji wataruhusiwa kuingia katikati ya jiji ili kusaidia kubeba abiria ambao wanamudu usafiri huo ili kusaidia wanaokwama kutokana na agizo la daladala kutosimamisha abiria. 

“Mnaruhusiwa kuingia mjini kwa kufuata sheria na taratibu za kutoingia kwenye barabara ya mwendo kasi na mnatakiwa kuvaa elementi unapokuwa kwenye chombo chako, zoezi hili litaendelea hadi corona itakapoisha. 

“Tunachotakiwa kufanya hivi sasa ni kusaidia wafanyakazi kuwahi kazini na kufanya shughuli kwa wakati ili tuweze kuepukana na hali ngumu ya maisha,” alisema Makonda. 

Vilevile aliwataka wazazi kutulia nyumbani kama hawana safari za lazima ili kuepusha kusababisha maambukizi ya corona kuleta nyumbani na kuathiri familia. 

Pia Makonda ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (Latra), kuhakikisha ifikapo leo saa 6:00 mchana wawe wameshabadilisha ruti za magari kuwa fupi. 

“Magari kuwa na ruti ndefu ndio sababu mojawapo ya abiria wa vituo vya katikati kukosa usafiri, unakuta abiria wamepanda kutoka Mbagala hadi Ubungo abiria wengine wanakosa pa kukaa. 

“Naomba Latra wakae na wamiliki wa magari na wakubaliane kubadilisha ruti ziwe fupi fupi kama Buruguni hadi Ubungo, hadi kesho (leo) saa 6 wasipobadilisha ruti saa saba mchana nitatangaza na kubadilisha ruti mimi mwenyewe,” alisema Makonda. 

 ELIMU YA CORONA 

Katika hatua nyingine, Taasisi isiyo ya kiserikali ya Walter Nnko Foundation (WNF) imejitolea kupita mitaani na kugawa vifaa na kutoa elimu kuhusu corona. 

Akizungumza na MTANZANIA jana Dar es Salaam, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk. Walter Nnko, alisema ameamua kujitolea kuwasaidia wananchi ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na Covid-19. 

“Nilishaanza kutoa elimu katika Jiji la Dar es Salaam, naangalia hasa maeneo ya sokoni na stendi ambako watu wanaendelea na shughuli zao, na mwitikio wa watu kufuatilia elimu hii ni mkubwa. 

“Matarajio yetu ni kuona kila mmoja ajue madhara ya ugonjwa huu na jinsi gani ya kujikinga ili taifa letu lisiingie kwenye janga la kuwa na wagonjwa wengi,” alibainisha Nnko. 

Alishauri taasisi mbalimbali binafsi na za umma kutoa elimu ya kutosha kwa jamii kuhusu Covid-19. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles