Elizabeth Kilindi, Njombe.
Mgombea ubunge Jimbo la Ludewa mkoani Njombe kwa tiketi ya chama cha mapinduzi (CCM), Wakili Joseph Kamonga, ametaja vipaumbele tisa atakavyovisimamia na kuvitekeleza endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu Oktoba 28 mwaka huu.
Kamonga alivitaja vipaumbele hivyo mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa kampeni za Jimbo la Ludewa ulifanyika katika viwanja vya shule ya msingi Itundu kata ya Mlangali uliudhuriwa na viongozi wa chama mkoa na wilaya na kuvitaja vipaumbele hivyo kuwa ni madini, miundombinu, afya, kilimo, mifugo, uvuvi, ajira kwa vijana na elimu.
Akizungumza katika uzinduzi huo Kamonga alisema atatuwatumikia wananchi wote bila kubagua na kwamba atakwenda kuisumbua serikali kuhusu mradi wa makaa ya mawe ya Liganga ambayo ni hazina kubwa kwa taifa na wananchi wa Ludewa.
‘’Udhamini ulifanyika mwaka 2015, fidia bado hazijalipwa kwa hiyo nitajitahidi sana kuisumbua serikali kwanza kuhakikisha fidia zinalipwa, unajua miradi haijaanza kutokana na uzalendo wa jemedari wetu Dk. John Magufuli alivyoona ule mkataba hauna maslahi kwa wananchi wa Ludewa ndo maana tunaona miradi imechelewa.
”Lakini kwa uzalendo wake huo sisi tutakwenda kumuomba aweze kulipa fidia wananchi wale kwasababu zile ni takribani bilioni 12, mniambie jamani bilioni 12 zikimwagika Ludewa si tutabadilika sana kwa hiyo nitafuatilia wale wananchi baada ya kuwazuia kufanya shughuli zao za kiuchumi na uzalishaji mali waweze kulipwa fidia ili waache yale maeneo mikononi mwa serikali, alisema Kamonga
Aidha Kamonga aliongeza kuwa atahakikisha ujenzi wa chuo cha ufundi stadi VETA Shaurimoyo kinakamilishwa ili vijana wa Ludewa waweze kusoma na kupata ujuzi mbalimbali ambao utawasaidia kupata ajira.
‘’Najua Ludewa ina vijana wengi ambao hawana ajira nilikua napitia ilani ya CCM nimeona mambo mazuri kuna mkakati wa kusaidia vijana, wanawake na makundi maalumu ile mikopo tunakwenda kuhakikisha itolewa, vikundi mbalimbali vinaundwa na kuimarisha shughuli mbalimbali za ujasiriamali kwa vijana, wakinamama na hata wazee, ’’alisema Kamonga.
Katika uzinduzi huo wanachama wa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema) kata ya Mlangali wapatao 27 walikihama chama hicho na kutimkia CCM.