Berlin, Ujerumani
WAKATI vita ikiendelea nchini Libya, jitihada zinazofanywa kikanda na kimataifa za kuikomesha katika nchi hiyo zimeingia katika awamu mpya.
Mgogoro huo wa Libya sasa unajadiliwa kwenye mkutano wa amani wa Berlin ulioandaliwa kwa lengo na madhumuni ya kutafuta njia ya kisiasa ya kuutatua.
Mkutano huo ulifanyika Jumapili katika mji mkuu huo wa Ujerumani, huku viongozi wa pande mbili hasimu nchini Libya; Fayez al-Sarraj na Khalifa Haftar wakiwa ni wahudhuriaji tu na si washiriki rasmi wa mkutano huo.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alisema wameanzisha mchakato mpya ili uwe ni chachu ya tumaini kwa watu wa Libya.
“Lengo letu ni kuunga mkono mpango wa Umoja wa Mataifa. Tunakubaliana kwa kauli moja kuwa tunahitaji njia ya ufumbuzi wa kisiasa nchini Libya na hakuna nafasi yoyote kwa utumizi wa nguvu za kijeshi, kwa sababu njia ya utatuzi wa kijeshi inazidisha machungu na mateso wanayopata wananchi wa Libya,” alisema.
Washiriki wa mkutano wa Berlin walitilia mkazo ulazima wa kuheshimiwa marufuku ya uingizaji silaha nchini Libya na kuchukuliwa hatua madhubuti zaidi za kusimamia suala hilo katika siku za usoni.
Vikosi vitiifu kwa Khalifa Haftar, vinavyojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) ambavyo vinadhibiti eneo la mashariki ya nchi hiyo na ambavyo vimeanzisha hujuma na mashambulio kwa muda mrefu ya kutaka kuudhibiti mji mkuu Tripoli na kuunda Serikali kuu nchini humo, vimeshadidisha mashambulio yake dhidi ya mji huo na miji mingine muhimu kadhaa.
Hali hiyo imesababisha kuongezeka uingiliaji wa nchi washirika katika masuala ya ndani ya Libya, ambapo nchi za kigeni na Saudi Arabia zinamuunga mkono rasmi Khalifa Haftar na hatua zinazoendelea kuchukuliwa hivi sasa na wapiganaji wake zimepata baraka kamili na uungaji mkono wa kifedha na silaha wa nchi hizo.
Baadhi ya duru zimeripoti kuwa zaidi ya askari 700 wa kigeni wametumwa nchini Libya na ndege za kivita za Abu Dhabi zimeshambulia baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.
Hali hiyo iliifanya Serikali ya mapatano ya kitaifa ya Libya, nayo pia iamue kuomba msaada kwa Uturuki ili kuweza kulinda nafasi yake.
Kuhusiana na suala hilo, pande hizo mbili zimesaini mkataba wa ushirikiano wa kijeshi sambamba na Ankara kuafiki kutuma wanajeshi wake Libya.
Hata hivyo jambo hilo limelalamikiwa kimataifa pamoja na nchi majirani wa Libya.
Kushadidi mgogoro wa Libya kumeibua hatari ya kuongezeka harakati za makundi ya kigaidi na kusambaa katika eneo hilo, kusitishwa usafirishaji mafuta na gesi na taathira zake kwa soko la nishati na vile vile kushadidisha harakati za magenge ya magendo ya binadamu na kushamirisha uhamiaji haramu kuelekea Ulaya na maeneo mengine ya dunia.
Masuala yote hayo yamezifanya jumuiya na jamii ya kimataifa kwa ujumla ifanye juhudi maradufu za kusitisha mapigano na kutatua mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo ya kisiasa.
Kuhusiana na suala hilo, wiki iliyopita ilikuwa imepangwa kuwa Serikali ya mapatano ya kitaifa isaini makubaliano ya usitishaji vita wa muda na kiongozi wa kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya, Khalifa Haftar, lakini licha ya matarajio ya kimataifa yaliyokuwepo, Haftar alikataa kusaini makubaliano hayo.
Hii ni pamoja na kuripotiwa kwamba vikosi vya kundi hilo la LNA vimeendeleza hujuma na mashambulio yao dhidi ya Tripoli.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ambaye naye pia alihudhuria mkutano wa Berlin, alisema kutokana na hali ilivyo hivi sasa nchini Libya kuna hatari ya kuongezeka mivutano ya kikanda; na kwa muktadha huo amezitaka pande zinazohusika moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika mapigano yanayoendelea zifanye kila ziwezalo ili kusaidia kuyasitisha kivitendo.
Ijapokuwa washiriki wote wa mkutano wa amani ya Libya uliofanyika mjini Berlin wamesisitiza kuwa hawatouunga mkono upande wowote katika mapigano na wakatilia mkazo kutafuta njia za ufumbuzi wa kidiplomasia, lakini hakuna matarajio makubwa ya kitendawili cha mgogoro huo kuweza kuteguliwa kwa vikao na mikutano kama hiyo.
Nafasi ya jiopolitiki ya Libya, uingiliaji wa kigeni, mivutano ya nyuma ya pazia ya kuwania utajiri wa nchi hiyo na vile vile maslahi ya makundi ya ndani na nchi jirani, yote hayo ni kikwazo na kizuizi kikubwa kinachokwamisha kupatikana suluhu na amani nchini humo; na ndiyo maana vita vya kuwania madaraka vinaendelea kushuhudiwa katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Hapana shaka hali itaendelea kuwa hivyo isipokuwa tu kama makundi ya kisiasa na kijeshi ya nchi hiyo yatatanguliza mbele maslahi ya kitaifa na ya nchi yao badala ya manufaa yao binafsi ya kupigania madaraka na kuamua yenyewe kubuni njia ya kuhitimisha mgogoro huo.