24.7 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

MGODI WA ACACIA KUHAKIKIWA UPYA

Na HARRIETH MANDARI- GEITA


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ametangaza kuhakikiwa upya   maeneo yote ya migodi nchini.

Amesema  timu ya watalaamu itaanza kazi hiyo kwenye mgodi wa dhahabu wa Kampuni ya Acacia uliopo Nyamongo Tarime mkoani Mara.

Majaliwa amesema ikiwa maeneo yaliyopatiwa leseni,  wahusika wataonekana wameshindwa kuyaendeleza tangu yaliposajiliwa,  watanyang’anywa na kupewa watu wengine kwa mujibu wa sheria.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akifunga maonyesho ya kwanza ya kimataifa yaliyofanyika kwa wiki moja mkoani Geita, ambayo yalihusisha wadau wa sekta ya madini, wafanyabiashara na taasisi za fedha zikiwamo benki mbalimbali.

“Tayari hatua ya kuhakiki na kutathimini  wamiliki wa  leseni  za maeneo tengefu  na makubwa ya uchimbaji na ambao kwa miaka mingi tangu kupatiwa leseni hawajachimba, watanyang’anywa na  watapatiwa  wachimbaji wadogo na wa kati ambao wako tayari kuchimba ili siyo tu wajiinue kiuchumi lakini pia kuliingizia taifa mapato,” alisema Majaliwa.

Uamuzi huo wa Serikali umetolewa  huku   Kampuni  Acacia ikiendelea   kuzuiwa   kusafirisha   makinikia   tangu Machi mwaka jana.

Imeelezwa kuwa hatua hiyo imeisababisha hasara    ya Dola za Marekani milioni 19.1 (zaidi ya Sh bilioni 43) kampuni hiyo.

Akizungumzia matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na wawekekzaji wa madini kwa ajili ya miradi ya maendeleo (CSR),  Majaliwa alisema Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amekwisha kuanza kufanya ukaguzi nchi nzima.

“Kwa wale watakaopatikana na ubadhirifu au  matumizi mabaya ya fedha hizo za maendelelo hatua kali zitachukuliwa  dhidi yao,”alisema.

Aliwataka wachimbaji wadogo wa madini kwenda benki wakakope mitaji kwa sababu wana uhakika wa kudhaminiwa na Benki Kuu ya Tanzania.

“Msihofu kukopa, kukopa ni jambo la kawaida. Nenda mkakope   mpate mitaji ya kununua mitambo ya kuchenjua dhahabu na madini mengine,” alisema.

Waziri Mkuu alisema  wakati akikagua mabanda ya maonyesho kwenye viwanja hivyo, alielezwa kwamba gharama ya mtambo unaohitajika kwa wachimbaji wa kati inafikia Sh milioni 10.

“Naomba niwaeleze wanaGeita kwamba mnakopesheka, nendeni mkaombe mikopo mnunue mitambo ya kuchenjua dhahabu,” alisistiza.

Hata hivyo, Majaliwa aliwataka wananchi wa Geita kutambua  kwamba siri kubwa ya kufanikiwa kupata mikopo ni kwa wao kuunganisha nguvu kwa kujiunga kwenye vikundi  wawe na malighafi ya kutosha mitambo hiyo.

“Wakuu wa wilaya za mkoa huu simamieni hatua hii kwa sababu wilaya zenu zote zinachimba madini. Simamieni uundaji wa vikundi na mwende mkawasemee benki  wanapokwama,” alisema.

Akielezea kuhusu makusanyo ya fedha kutokana na mauzo ya dhahabu kwenye mkoa huo, Waziri Mkuu alisema tangu Aprili mwaka huu, mapato yanayotokana na madini yameongezeka kutoka Sh milioni 400 na kufikia Sh milioni 850 Agosti, mwaka huu.

Waziri Mkuu pia amewataka wazazi wawapeleke watoto wao kwenye vyuo vya ufundi vya stadi vinavyomilikiwa na Mamlaka ya Ufundi Stadi Tanzania (VETA)  wakajifunze taaluma ya uchongaji wa madini na vito kama eneo jipya la ajira nchini.

“Nimemuona binti mmoja kwenye banda la VETA akielezea vizuri kuhusu uchongaji wa madini na vito. Nikabaini kumbe jambo hili linaweza kufanyika nchini kwetu.

“Ninawasihi wazazi pelekeni watoto wenu kwenye vyuo vya VETA vya Mwanza, Geita na Moshi ambako kozi hii inafundishwa,” alisema Majaliwa.

Awali, akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Madini, Angella Kairuki alisema sekta ya madini ilichangia pato la taifa kwa asilimia 4.8 tu ingawa sekta hiyo iliongoza kwa kuingiza fedha za kigeni kutokana na bidhaa zinazouzwa nje ya nchi mwaka 2016/2017.

Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha sekta hiyo inachangia pato la taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

Alisema zaidi ya asilimia 90 ya thamani ya madini yanayouzwa nje ya nchi ni dhahabu na Mkoa wa Geita unaongoza kwa uzalishaji wa dhahabu ambako katika mwaka 2017 asilimia 41.2 ya dhahabu iliyouzwa ilitoka kwenye mkoa huo.

“Kwa upande wa wachimbaji wadogo wanaozalisha dhahabu, Mkoa wa Geita unaongoza ambako tani 1.175 za dhahabu zenye thamani ya Sh bilioni 89 zilizalishwa, na kati ya hizo asilimia 49 ilizalishwa na wachimbaji wadogo,” alisema Kairuki.

Alisema takwimu hizo zilipatikana kabla Serikali haijachukua hatua ya kuzuia usafirishaji wa carbon yenye dhahabu kuvuka mipaka ya mkoa.

Hali hiyo ilikuwa inachangia utoroshaji, ukwepaji wa kodi na jamii husika kushindwa kunufaika na madini yaliyopo kwenye maeneo yao, alisema.

Waziri   alisema  juhudi zinafanyika na serikali  kuboresha uchimbaji ambako vituo vinne vimeanza kujengwa katika mikoa minne nchini.

Alisema  kimoja kitakuwa  Bukombe mkoani Geita na kuwataka wachimbaji kuchangamkia mafunzo hayo mara  vitakapoanza kutoa huduma hiyo.

Maonyesho hayo yalikutanisha makampuni 250 kutoka maeneo mbalimbali  nchini na yataendelea hadi Oktoba 3, 2018 kutokana na ombi la Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel kwa Waziri Mkuu.

Naye  Mkuu wa Mkoa wa Geita,   Robert Gabriel, alisema wakati umefika kwa mkoa huo kuwa na hadhi ya kuzalisha   dhahabu.

Alisema  mikakati imeanza kutekelezwa  kuhakikisha  fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatumika ipasavyo.

“Tayari miradi mbalimbali imeshaanza kutekelezwa ikiwamo ujenzi wa zahanati katika kila kijiji, ambao unadhaminiwa na makampuni ya uchimbaji dhahabu ya Acacia na  GGM  na ifikapo mwaka kesho mradi utakua umekamilika,” alisema.

Alisema tangu kampeni ya ujenzi  wa zahanati hizo ambazo nyingine tayari zimekamilika,   kumekuwa na ongezeko  kutoka asilimia 23  hadi   asilimia 93.

“Kabla ya mradi huo kulikuwa na vifo vya wastani wa kina mama 80 na watoto   mwaka  jana  kutokana na upungufu wa zahanati.

“Hivyo tuna uhakika   mradi huu utakapokamilika  idadai hiyo itakwisha kama siyo kupungua,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles