NA HASTIN LIUMBA
-NZEGA
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja amemuomba Mke wa Rais Mstaafu, Mama Salma Kikwete kuutafakari kwa makini uteuzi wa ubunge alioteuliwa jana na Rais John Magufuli.
Mgeja ambaye pia ni Mwenyekiti wa taasisi inayoshughulika na utawala bora ya Tanzania Mzalendo Foundation, amesema nafasi aliyofikia mama Salma akiwa mke wa rais mstaafu na ‘First Lady’ wa nchi ni nafasi kubwa kiitifaki hivyo anapaswa kuwa na heshima na abakie kuwa mama mshauri na mlezi wa taifa.
“Namuomba Mama Kikwete aige mfano wa mama Regina Lowassa (mke wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa) ambaye wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015 na baada ya uchaguzi Chadema ilimpa heshima kwa kumteua kuwa Mbunge wa Viti Maalumu lakini kwa heshima aliikataa nafasi hiyo.
“Mke wa rais mstaafu siyo mtu au kiongozi mdogo lazima tujiulize inapotokea akachangia hoja ndani ya bunge ikapingwa au aambiwe kaa chini au toka nje au atolewe nje na askari wa bunge je, hiyo heshima au aibu na fedheha inaenda kwa nani?” amehoji Mgeja.
Pamoja na mambo mengine, Mgeja amesema wake wa viongozi ni sehemu ya viongozi ambapo ana mashaka itifaki ndani bungeni inaweza kugongana hivyo amemtaka Mama Salma Kikwete akapokea ushauri na mitazamo ya watu mbalimbali na isimaanishe kwamba anamuonea wivu kwani maamuzi yanabaki kwake kukataa ama kukubali ushauri huo kama changamoto katika kupanga na kuchagua.