NA AZIZA MASOUD,
WATOTO wanapozaliwa huwa wanapitia hatua mbalimbali za makuzi, kila hatua anayopitia ama kupaswa kuipitia mtoto ina umri wake pamoja na changamoto zake.
Hatua za watoto kukua huanza kwakuona na kutambua watu wanaomzunguka kupitia harufu zao, hili hufanyika mtoto anapokuwa na umri kuanzia mwezi mmoja.
Mbali na hatua hiyo, pia kuna hatua mbalimbali za makuzi ambazo anapitia mtoto, ikiwamo   umri wa kujitambua na kuanza kufanya mambo mbalimbali mwenyewe, ikiwamo kwenda haja mwenyewe bila msaada wa mzazi.
Wazazi ama walezi wengi wanachukizwa na tabia za watoto, hasa anayeonekana kuanza kujitambua kujisaidia kwenye nguo.
Ukiachana na hao wanaojitambua, wapo wazazi ambao wamefanikiwa kuwafundisha watoto wao wadogo usafi kulingana na malezi waliyowapa ambapo mtoto anakuwa hapendi kujisaidia kwenye nguo.
Watoto wenye tabia za usafi hata wakiwa na umri mdogo siku zote wanapobanwa na haja pamoja na kuwa hawawezi kusema huanza kulia, akifikia hatua hiyo mzazi muelewa anakuwa anajua mtoto anahitaji nini na kuanza kumvua nguo ili aweze kujisaidia.
Ukifanikiwa kumtengenezea mazoea mazuri mtoto pia itamsaidia kwa baadaye kuweza kujielekeza na atakapofikia umri wa kujitegemea kati ya miaka miwili mpaka mitatu anakuwa tayari ameshajijengea utaratibu wa kujisaidia mwenyewe.
Mzazi unapaswa uanze kumwelekeza mtoto sehemu za kujisaidia ambapo wapo ambao huanza kujisaidia kwa kutumia poti na kama atakuwa amefikia umri wa kujisaidia chooni moja kwa moja, lengo ni kuhakikisha hajisaidii kwenye nguo.
Mtoto anapopata uelewa wa kuvua nguo na kujisaidia katika eneo husika utamsaidia kuwa na uwezo wa kudhibiti haja ndogo na kubwa pamoja na kuacha matumizi ya nepi.
Mbali na hilo, pia mtoto anapopata uelewa wa kuhusu eneo la kujisaidia itamsaidia kuwa katika hali ya usafi kwa sababu katika kipindi chote atakachokuwa amepata uelewa hataweza kujisaidia kwenye nguo.
Ili kuepuka hali hiyo, watoto wanapofikia umri huo wazazi wengi wanakuwa wanajitahidi kuwaelekeza watoto kujitegemea na namna ya kujizuia anapokuwa anahisi kujisaidia haja ndogo ama kubwa.
Hii pia ni hatua muhimu katika maendeleo ya mtoto na inahitaji subira na kuwatia moyo.
Mzazi ni vema ukaanza kumfundisha mtoto tabia ya usafi na kuchukia uchafu mapema, ili uweze kumjengea mazingira ya kuwa kijana mtanashati.