Kulwa Mzee, Dar es salaam
JAMHURI imefikisha mahakamani Mfanyakazi wa Benki ya CRDB tawi la Ubungo, Andrew Babu (27) na wafanyabiashara watatu, kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kuiba zaidi ya Sh milioni 100 za mteja katika akaunti.
Pia wanashtakiwa kwa kula njama, kughushi Tembo kadi ya mteja na kutakatisha zaidi ya Sh milioni 100 huku wakijua ni la fedha za makosa ya wizi.
Wakili wa Serikali Mwandamizi aliwataja washtakiwa, wengine katika kesi hiyo ni William Sige (52), Justina Boniphace (49) na Alli Tutupa (35) wote wakazi wa jijini Dar es Salaam.
Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Mbando, alidai kati ya Oktoba 2018 na Aprili 19, 2019 washtakiwa wote kwa pamoja walikula njama kutenda kosa la wizi.
Inadaiwa Oktoba 29, 2018 katika benki ya CRDB Tawi la Ubungo, ndani ya Manispaa ya Ubungo, mshtakiwa Babu peke yake kwa nia ya kulaghai au kudanganya, alighushi sahihi ya Charles Kihamia katika fomu ya maombi ya Tembo card.
Pia mshtakiwa Babu anadaiwa, Novemba 6, 2018 alighushi sahihi ya Kihamia katika kitabu cha usajili kwa madhumuni ya kuonyesha kuwa, sahihi hiyo imewekwa na Kihamia huku akijua kuwa siyo kweli.
Mshtakiwa Babu anadaiwa Novemba 5, 2018 alighushi sahihi ya Kihamia katika usajili wa kadi ya visa ya Tembo, kwa madhumuni ya kuonesha kuwa sahihi hiyo imewekwa na Kihamia huku akijua si kweli.
Inadaiwa Novemba 6, 2018 alighushi sahihi ya Kihamia katika kitabu cha usajili wa uelekezaji kwenye fomu ya maombi kwa madhumuni ya kuonesha kuwa, sahihi hiyo imewekwa na Kihamia huku akijua kuwa si kweli.
Mshtakiwa Babu pia anadaiwa, Oktoba 29, 2018 huko katika benki ya CRDB, alitoa fomu ya kughushi ya maombi ya Tembo kadi kwa ofisa wa banki hiyo aitwaye Omary Mduyah kwa dhumuni la kuonesha kuwa fomu hiyo imetolewa na kusainiwa na Kihamia huku akijua si kweli.
Katika shtaka la mwisho, inadaiwa kati ya Novemba 7, 2018 na Aprili 29,2019 washtakiwa hao kupitia kadi ya gold ya Visa, walijipatia Sh. 106,267,907/- kutoka kwa Charles Kihamia kupitia Visa gold card huku wakijua kuwa fedha hizo ni mazao ya makosa tangulizi ya kughushi na wizi.
Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, kesi imeahirishwa hadi Oktoba 10.