Azaki zataka viongozi wa dini kutoegemea chama chochote

0
494

Asha Bani -Dar es salaam

VIONGOZI wa dini wametakiwa kuhubiri amani  kwa waumini wao na kujiepusha na kauli zenye kupendelea mgombea au chama fulani wawapo kwenye maeneo ya ibada na kwenye hadharani katika kipindi cha kuelekea kwenye Uchaguzi za Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Wito huo ulitolewa jana jijini Dar es Salaam na Muunganiko wa Asasi za Kiraia nchini (Azaki), wakati wakizungumza na waandishi wa habari juu uzinduzi wa Ilani ya Uchaguzi ya Asasi za Kiraia ya Mwaka 2019/2020 inayotarajiwa kuzinduliwa leo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Ushirikiano na Maendeleo ya Vijana (YPC),  Israel Ilunde,  alisema kumekuwa na matukio mengi ambayo hutokea katika kipindi cha uchaguzi ambapo viongozi wa dini wanajihusisha na kutoa matamko yanayolenga kupendelea chama kimoja.

Aliwashauri katika kipindi hicho viongozi wa dini pia wanapaswa kuonya, kukemea na kupaza sauti dhidi ya aina zozote za vitendo vya ukiukwaji wa sheria kwa waumini au wasimamizi wa uchaguzi.

Ilunde alisema viongozi hao ni nguzo muhimu katika ustawi wa nchi hivyo wanapaswa kukemea vitendo vyote vitakavyosababisha vurugu na uvunjifu wa amani ya nchi wakati wa kuelekea uchaguzi.

Hata hivyo alisema kutokana na changamoto zilizotokea mwaka 2015, ikiwemo ukosefu wa fedha za kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchaguzi, Azaki  zinapaswa kujiandaa mapema kwa kutafuta rasilimali na kufanya taratibu zingine za kisheria ili waweze kushiriki katika chaguzi kikamilifu.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Utoaji wa Taarifa kwa wananchi, Deus Kibamba, alisema lengo ya ilani ya AZAKI ni kuwasaidia Watanzania kubainisha vipaumbele vikuu watakavyotumia kuchagua viongozi wenye uwezo wa kuvitekeleza na kuweka vipaumbele hivyo vya Watanzania katika lugha rahisi kwa ajili ya kushawishi wagombea na vyama kama agenda zao kabla na baada ya uchaguzi.

Kwa upande wake Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, alisema nia ya ilani hiyo ni kutoa mwongozo kuhusu namna ambavyo vyama vya siasa, wagombea, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),  vyombo vya usalama, Serikali, Azaki na wananchi wanatakiwa kushiriki katika uchaguzi kwa amani, utulivu na uhuru ili kufikia malengo ya kuwapata viongozi wanaowataka.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Mlango wa Matumaini Tanzania,  Clemence Mwombeki, alisema malengo mengine ya ilani ni kutoa mwongozo kwa Serikali, vyama vya siasa, wagombea, wapiga kura na viongozi watakaoshinda chaguzi ili kutambua matakwa ya sheria, kijamii na kidemokrasia katika kutekeleza wajibu wao kwa manufaa ya Taifa na watu wake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here