Kulwa Mzee na Elizabeth Joachim, Dar es Salaam
Mfanyabiashara, Akram Azizi amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na makosa 75 ya uhujumu uchumi, likiwemo la kukutwa na nyara za Serikali na utakatishaji fedha kiasi cha dola za marekani 9018 ambazo ni zaidi ya Sh.Milioni20 za Kitanzania.
Anashtakiwa kwa uhujumu uchumi kwa kukutwa na nyara za serikali, silaha 70, risasi 6496 na kutakatisha fedha ambapo alikutwa na Dola za Marekani 9018.
Mshtakiwa huyo alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Augustin Rwizile.
Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi alidai mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo kati ya Juni na Oktoba 30 mwaka huu maeneo ya Oysterbay.
Kadushi alidai mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka 70 ya kukutwa na silaha, mawili ya kukutwa na risasi, mawili ya kukutwa na nyara za Serikali na moja la utakatishaji wa fedha Dola za Marekani 9018.
Hata hivyo licha ya kusomewa mashitaka hayo yanayomkabili lakini hakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi huyo.
Wakili Kadushi alidai upelelezi haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 12 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa tena ili kujua kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.
Mfanyabiashara huyo ambaye ni mdogo wa Rostam Azizi anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 82/2018.