KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
ALIYEKUWA Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Julai 28 mwaka huu anatarajia kuanza kujitetea dhidi ya mashtaka ya kutumia lugha matusi dhidi ya Rais John Magufuli.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imefikia uamuzi huo jana wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya utetezi lakini haikuendelea.
Mshtakiwa Halima aliifahamisha Mahakama kwamba Wakili wake, Hekima Mwasipo, anaumwa hivyo aliomba kesi iahirishwe.
Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, alikubali maombi hayo na kuamuru kesi iahirishwe hadi Julai 28 ambapo mshtakiwa ataanza kujitetea.
Mshtakiwa anakabiliwa na shtaka moja la kutumia lugha ya matusi dhidi ya Rais John Magufuli.
Inadaiwa Julai 3 mwaka 2017 maneno ya Makao Makuu ya Chadema, mshitakiwa alitumia lugha ya matusi dhidi ya Rais Magufuli akisema ‘anaongea hovyo hovyo anatakiwa afungwe breki’.
Awali Februari 20 mwaka huu upande wa Jamhuri katika kesi hiyo ya uchochezi, walifunga ushahidi wakiwa na mashahidi watatu.
Katika kesi hiyo, inadaiwa Julai 3,2017 katika Makao Makuu ya Ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yaliyopo Mtaa wa Ufipa Wilaya ya Kinondoni, Mdee alitamka maneno dhidi ya Rais John Magufuli kuwa “anaongea hovyohovyo , anatakiwa afungwe breki” na kwamba kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Mdee alifikishwa mahakamani hapo Julai 10, 2017 na yupo nje kwa dhamana.