29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Ajali ya basi yaua watatu, kujeruhi 25

Janeth Mushi, Arusha

WATU watatu wamefariki dunia huku wengine 25 wakijeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Coastline lililokuwa likitokea Musoma kwenda Arusha, kupata ajali huku chanzo kikitajwa ni uzembe wa dereva.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhan Kingai, ajali hiyo ilitokea Juni 24 saa 10:30 jioni, katika eneo la Kilimatembo, Kata ya Rhotia wilayani Karatu.

Alisema gari hilo lililokuwa na namba za usajili T 405 AME aina ya Scania, lililokuwa likiendeshwa na na dereva ambaye jina lake halijafahamika, liliacha njia na kupinduka baada ya kugonga ngema upande wa kulia wa barabara.

Alisema waliofariki ni mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka (40-45), mwanaume mwenye umri kati ya (30-40) na mtoto mwenye umri wa miezi sita ambao walifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya KKKT Karatu.

“Aidha majeruhi saba waliruhusisa baada ya kupata matibabu, wengine 18 ambao ni wanaume nane na wanawake 10 bado wamelazwa katika hospitali hiyo na wengine hali zao ni mbaya na taratibu za kuwahamishia katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru Arusha zinaendelea,”alisema

Taarifa hiyo ya polisi ilidai chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kutochukua tahadhari za kutosha katika eneo hilo lenye mteremko mkali na baada ya ajali kutokea dereva huyo alitoroka na juhudi za kumtafuta zinaendelea ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

“Nitoe wito kwa madereva kuwa makini na kuchukua tahadhari za usalama barabarani pindi wanapotumia vyombo vya moto ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea, wasafiri wakiona mienendo isiyo mizuri kwa madereva watoe taarifa kwa polisi ili tuchukue hatua kabla ajali haijatokea,” ilisema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,609FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles