Kulwa Mzee -Dar es salaam
WABUNGE watatu wa Chadema akiwemo Halima Mdee (Kawe) na wenzao 23 wamepanda kizimbani wakikabiliwa na mashtaka saba ikiwemo kuharibu geti kuu la kuingia gerezani na kumchania shati askari Magereza aliyekuwa analinda katika geti hilo.
Washtakiwa hao walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi na kusomewa mashtaka na jopo la mawakili wa Serikali likiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Renatus Mkude.
Washtakiwa wengine ni pamoja na Ester Bulaya (Bunda Mjini), Jesca Kishoa (Viti Maalumu), Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, Patrick Asenga, Henry Kilewo, Yohana Kaunya, Mshewa Kaluwa, Pendo Raphael, Cesilia Michael, Happy Abdallah, Steven Kitomari na Paul Makali.
Akisoma mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Renatus Mkude alidai washtakiwa walitenda makosa hayo Machi 13 mwaka huu katika Gereza la Segerea.
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa walikaidi amri halali ya askari namba B3648 Sajent John iliyowataka kuondoka kwa amani eneo hilo na kuliacha likiwa salama.
Shtaka la pili wanadaiwa tarehe na mahali hapo hapo, washtakiwa walifanya mkusanyiko usio halali na kusababisha hali isiyokuwa ya kawaida kwa majirani na kuleta hofu iliyosababisha kuondoka kwa amani.
Washtakiwa wote wanakabiliwa na mashtaka ya kuharibu mali ambapo wanadaiwa kwa kushirikiana waliharibu geti kuu la kuingia katika gereza hilo mali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Shtaka la nne, tano na sita linawakabili washtakiwa Mdee, Bulaya na Jacob ambao wanashtakiwa kwa kutumia lugha ya kuudhi kwa Sajenti John.