Kulwa Mzee, Dar es Salaam
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu kwenda jela mwaka mmoja, Mchungaji Kanisa la The Hill Lord, David Chirhuza (33) na wake zake wawili kwa kosa la kuingia nchini bila kibali.
Aidha, imemhukumu Mchungaji peke yake kwenda jela mwaka mmoja kwa kufanya kazi ya uchungaji bila kibali cha makazi.
Mapema leo asubuhi, mahakama hiyo iliwatia hatiani Mchungaji huyo na wake zake wawili na mdogo wake baada ya kukiri kuingia nchini bila kibali na kufanya kazi ya uchungaji bila kibali cha makazi kabla ya kuahirishwa kwa muda na kutoa adhabu hiyo.
Washtakiwa hao wametiwa hatiani leo Jumanne Septemba 10, saa tatu asubuhi mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustino Mmbando na kusomewa mashtaka mawili.
Washtakiwa ambao ni wake wa Mchungaji ni Esther Sebuyange (27), Kendewa Ruth (26) na Mshtakiwa mwingine mdogo wa Mchungaji, Samuel Samy (22).
Wakili wa Serikali kutoka Uhamiaji Godfley Ngwijo akisaidiana na Sitta Shija, wakisoma mashtaka kwa nyakati tofauti walidai kwamba, Septemba 2 mwaka huu eneo la Salasala Kilimahewa, Dar es Salaam, mchungaji huyo na wenzake walibainika kuingia nchini bila kibali.
Katika shtaka la pili, ilidaiwa mchungaji huyo pekee alibainika kujihusisha na kazi za kanisa akiwa hana kibali cha makazi.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Mchungaji David alikiri shtaka la kwanza la kuingia nchini bila kibali na kukiri shtaka la pili kufanya kazi ya uchungaji huku akiwa hana kibali cha makazi.
Washtakiwa wengine walikiri shtaka la kuingia nchini bila kibali. Mahakama ilikubali kuwapa dhamana kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao ni watumishi wa Serikali wenye barua na kitambulisho.
Washtakiwa wote waliomba mahakama iwasamehe, isiwape adhabu kali, Mchungaji alisema kazi alivyokuwa akiifanya ya kuhudumia jamii si biashara pia kusimamia sheria ya Mungu.