NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Iringa mjini, Peter Msigwa (Chadema), anayekabiliwa na kesi ya uchochezi na wenzake wanane  akiwamo Mwenyekiti   Freeman Mbowe, hajapata wakili wa kumwakilisha mwezi sasa.
Msigwa alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde, ambaye aliskiliza kesi hiyo jana kutokana na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, anayeisikiliza kuwa likizo.
Akijiwakilisha mwenyewe, Msigwa alisema  hadi sasa hajapata wakili hivyo aliiomba mahakama muda   aweze kupata wakili wa kumtetea katika kesi hiyo.
Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo  ni Mbowe, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba John Mnyika.
Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Vincent Mashinji, ambao  wanatetewa na wakili Peter Kibatala.
Wakili wa Serikali, Simon Wankyo alidai   kesi ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali (PH) na kwamba Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri anayeisikiliza kesi hiyo yupo likizo.
Wankyo alisema kuna rufaa namba 215 ya mwaka huu Mahakama ya Rufaa iliyofunguliwa na washtakiwa ambayo inatarajiwa kutolewa uamuzi wiki ijayo katika tarehe ambayo watajulishwa hivyo aliiomba mahakama kuipanga kesi hiyo Oktoba 8.
Wakili Kibatala kwa upande wake, aliiomba mahakama iwapatie muda wa kutosha wateja wake, aliomba kesi ipangwe Oktoba 25,   mshtakiwa Msigwa naye aweze kutafuta wakili wa kumtetea.
Hakimu Kasonde alikubaliana na ombi la kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 25 kumpa muda wa kutosha Msigwa kutafuta wakili wa kumtetea na tarehe hiyo washtakiwa watasomewa maelezo ya awali.
Msigwa anatafuta wakili wa kumtetea baada ya wakili Jeremiah Mtobesya aliyekuwa akimtetea kujitoa   katika kesi hiyo.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.