24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mchezo mchafu kesi za dawa za kulevya

MADAWANa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KESI 18 za dawa za kulevya zilizokuwa zikisikilizwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam zinafutwa kwa sababu zilisajiliwa kimakosa katika katika mahakama hiyo na washtakiwa wanapandishwa upya kizimbani.
Hayo yalibainika jana baada ya kesi nne kufutwa na kufanya idadi ya kesi hizo kufikia nane baada ya nne nyingine kufutwa juzi, ambapo washtakiwa walisomewa upya mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Kesi zote zinazofutwa matukio yalitokea kati ya mwaka 2010 na 2011, ambapo upelelezi ulishakamilika na zilipelekwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kuendelea kusikiliza ushahidi.
Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Godfrey Nzowa, alipoulizwa kuhusu kufutwa mfululizo kwa kesi hizo, alisema kesi hizo zinazofutwa zipo katika orodha ya kesi zilizopo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wiki hii kwa ajili ya kusikilizwa.
“Kwa wiki hii tutafuta kesi 18 ambazo zilianza kufutwa nne juzi, na jana nne, ambapo tatu zimefikishwa Kisutu na moja imepelekwa mkoani Pwani.
“Kesi zinazofutwa zimebainika kusajiliwa Mahakama Kuu katika kitabu cha kesi za uhujumu uchumi, ni makosa, zinarudi upya mahakamani ili washtakiwa waweze kusomewa mashtaka, na kwa kuwa upelelezi ulikamilika, watasomewa maelezo ya awali na kurudishwa tena mahakamani,” alisema.
Kamishna Nzowa alisema leo wanatarajia kufuta kesi nyingine nne, kesho zitafutwa tatu na keshokutwa pia zitafutwa kesi tatu.
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, alisema kesi za dawa za kulevya zilizosajiliwa kimakosa na Mahakama Kuu katika kitabu cha kesi za uhujumu uchumi zitaendelea kufutwa.
“Zipo kesi nyingi na zitaendelea kufutwa kutokana na Mahakama Kuu kufanya makosa kuzisajili katika kitabu cha kesi za uhujumu uchumi,” alisema.
Katika hatua nyingine, washtakiwa watatu wa dawa za kulevya walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu jana wakikabiliwa na kesi tatu tofauti za kusafirisha dawa hizo.
Mshtakiwa Abdallah Mwalimu (32), ambaye ni mfanyabiashara, alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda na kusomewa shtaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Evetha Mushi.
Evetha alidai Februari 4, 2011, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, mkoani Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa akisafirisha pipi 54 za cocaine zenye thamani ya Sh milioni 28.7.
Mshtakiwa hakutakiwa kujibu shtaka hilo, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika hivyo Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 6, mwaka huu, kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.
Naye raia wa Nigeria, Livinus, jana alifikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Cocaine zenye thamani ya Sh milioni 32.2.
Wakili wa Serikali Mwandamizi Tadeo Mwenempazi, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande Lema, kuwa Machi 3, 2011, mshtakiwa alikutwa katika uwanja huo wa ndege, akisafirisha kete 54 za dawa hizo ambazo ni gramu 804.70.
Mwenempazi alidai upelelezi umekamilika na kesi imepangwa Machi 4, mwaka huu, kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.
Kesi nyingine ilikuwa inamkabili Abbas Gede (31), ambaye alisomewa shtaka la kuingiza pipi 77 za dawa za kulevya akitokea nchini Brazil.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Rose Chilongozi, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa, kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo, Mei 14, 2011, katika uwanja huo wa ndege. Alikutwa akiingiza nchini pipi hizo ambazo ni gramu 1171.76 zikiwa na thamani ya Sh milioni 58.6.
Rose alidai upelelezi umekamilika, hivyo mshtakiwa atasomewa maelezo ya awali Machi 4, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles