MCHEZAJI wa timu ya Trabzonspor ya nchini Uturuki, Salih Dursun, juzi alionesha maajabu ya mwaka baada ya kuchukua kadi nyekundu na kumuonesha mwamuzi Deniz Bitnel katika mchezo dhidi ya Galatasaray.
Tukio hilo lilitokea mara baada ya mwamuzi huyo kuwaonyesha kadi nyekundu wacheza watatu wa timu ya Trabzonspor kwa wakati tofauti, kutokana na utovu wa nidhamu, hivyo Dursun naye aliamua kumpokonya kadi mwamuzi huyo na kumuonesha.
Hata hivyo, baada ya Dursun kumuonesha kadi hiyo mwamuzi na yeye alitolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na utovu huo wa nidhamu ambao aliuonesha.
Hadi dakika 90 zinamalizika, Trabzonspor ilikuwa na pungufu ya wachezaji wanne kutokana na kuonesha kadi nyekundu na mchezo huo ulimalizika huku Galatasaray wakiwa mbele kwa mabao 2-1.
Wachezaji ambao walioneshwa kadi nyekundu katika mchezo huo ni Luis Cavanda, kiungo wao Ozer Hurmaci, beki wao Aykut Demir na Dursun, wakati huo nyota wa Galatasaray, Lukas Podolski na Wesley Sneijder walioneshwa kadi za njano