WASHINGTON, MAREKANI
MWANADIPLOMASIA wa Marekani nchini Ukraine, William Taylor, jana ametoa ushahidi mbele ya kamati ya ujasusi ya baraza la wawakilishi katika mchakato wa uchunguzi dhidi ya rais wa nchi hiyo Donald Trump.
Kesi hiyo imesikilizwa kwa mara ya kwanza jana kwa njia ya televisheni, kwa nia ya kumshitaki Trump bungeni.
Taylor alimhusisha moja kwa moja Trump na shinikizo la kampeni dhidi ya Ukraine ili kufanya uchunguzi utakaomnufaisha yeye binafsi.
Taylor na mwanadiplomasia mwingine George Kent walitoa ushahidi juu ya shinikizo lililotolewa na Trump na washirika wake, dhidi ya Ukraine kumchunguza hasimu wake wa Democratic, Joe Biden kuhusu shughuli za kibiashara za mwanae wa kiume nchini Ukraine.
Taylor aliliambia baraza la wawakilishi kwamba, wafanyakazi wenzake walisikia mazungumzo ya simu mnamo Julai 26 kati ya Trump na Gordon Sondland, ambapo Trump alimuuliza kuhusu uchunguzi huo na kujibiwa kuwa Ukraine wako tayari kuendelea.