Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TANZANIA ndiyo itakayoamua hatua za kuchukua kuiwezesha irudishiwe msaada wa dola milioni 473 za Marekani (Sh trilioni moja), maofisa wa Marekani wamesema.
Kutokana na hali hiyo, Tanzania imetakiwa kuamua kama itahitaji kupata fedha hizo hasa jinsi inavyoshughulikia masuala ambayo yanaibua maswali ukiwamo uchaguzi wa marudio Zanzibar na Sheria ya Mtandao.
“Serikali ya Tanzania inahitaji kuamua namna itakavyoshughulikia masuala ya wasiwasi yaliyoifanya iondolewe katika mpango wa kuisaidia,” Renee Kelly, msemaji wa Shirika la Changamoto za Milennia (MCC) alisema kupitia ujumbe wa barua pepe na kuongeza:
“Ni juu ya Bodi ya MCC pia kuamua iwapo hatua hizo zitakazochukuliwa na Serikali ya Tanzania zitatosha kuirudisha katika mpango wa shirika hili.”
Bodi ya MCC ilitangaza Machi 28 mwaka huu kwamba inasimamisha msaada wa dola milioni 473 kwa Tanzania kutokana na kutoridhishwa na uchaguzi wa marudio wa Machi 20 visiwani Zanzibar.
Shirika hilo la Marekani pia lilisema uongozi katika Tanzania unapaswa kuhakikisha unakuwapo uhuru wa kutoa maoni na kukusanyika, katika sheria yake ya uhalifu wa mtandao.
Kelly hakujibu maswali iwapo kurudishwa msaada kutazingatia kufanyika uchaguzi mpya na kufanya mabadilko katika sheria hiyo ya mtandao.
Fedha hizo zililenga kupanua upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuisaidia Tanzania itekeleze mpango kabambe wa mageuzi ya sekta ya nishati.
Mwaka 2012, Tanzania ilitangazwa kufuzu vigezo vya kuipatia msaada wa dola milioni 473, baada ya awali kupokea msaada wa dola milioni 698 zilizofadhili miradi ya usafirishaji, nishati na maji.
Mpango huo wa miaka mitano na Tanzania ulihitimishwa mwaka 2013 — ukiwa msaada mkubwa zaidi kupitishwa na MCC tangu mwaka 2004.
Nafasi ya Tanzania kama mpokeaji mkubwa wa misaada ya Marekani iko hatarini kutokana na uamuzi huo wa uongozi wa MCC.