26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge wa Ukonga afariki dunia usingizini

mwaiposaNA ARODIA PETER, DODOMA
MBUNGE wa Ukonga jijini Dar es Salaam, Eugen Mwaiposa (55), amefariki dunia usiku wa kuamkia jana mjini Dodoma akiwa usingizini.
Akitangaza msiba huo bungeni jana, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema Mwaiposa alifariki dunia akiwa nyumbani kwake eneo la Chadulu mjini hapa.
Alisema kwa muda mrefu mbunge huyo aliyeingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2010, alikuwa na tatizo la shinikizo la damu.
Wabunge walikuwa wakiendelea kuchangia bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge, Lediana Mng’ong’o ambaye ghafla alimkatiza mchangiaji kuzungumza na kumpisha kwenye kiti Naibu Spika Ndugai, ambaye alitoa taarifa za kifo cha mbunge huyo.
Ndugai, alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa uchunguzi zaidi wa wataalamu.
Alisema mwili wa marehemu utaagwa kesho mjini hapa baada ya ndugu wa marehemu kuwasili.
Kutokana na msiba huo, Ndugai alitangaza kuahirishwa kwa Bunge hadi keshokutwa na kuagiza Kamati ya Uongozi kukutana na wabunge watapatiwa taarifa kwa njia ya mtandao wa simu.
“Natumia kifungu cha 152 kuahirisha Bunge hadi Alhamisi saa 3:00 asubuhi,” alisema Ndugai.
Mwaiposa ni mbunge wa pili kufariki dunia kwa mwaka huu, akimfuatia Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba, aliyefariki dunia Februari 28.
Komba alifariki dunia katika Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu kutokana na kuugua shinikizo la damu.
TAARIFA ZA KIFO
Taarifa za kifo cha Mwaiposa zilianza kuwafikia baadhi ya wabunge ambao ni marafiki zake saa 6:00 mchana, akiwamo Beth Machangu, ambaye aliondoka bungeni kwenda nyumbani kwa marehemu eneo la Chadulu.
Waliporudi waliwataarifu wenzao wakati huo Bunge lilikuwa linaendelea kujadili hotuba ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, taarifa ya kamati pamoja na hotuba ya upinzani.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya wabunge zinasema kuwa habari za kifo cha mbunge huyo zilitoka kwa dereva wake baada ya kumpitia ili kumpeleka bungeni na kukuta nyumba imefungwa na alipogonga mlango hakujibiwa.

WABUNGE WAMLILIA
Nje ya Ukumbi wa Bunge makundi ya wabunge mbalimbali walikuwa wakijadiliana na hata kuzungumzia kifo cha mbunge mwenzao.
Mbunge wa Viti Maalum, Rita Kabati (CCM) aliliambia MTANZANIA kuwa ameshtushwa na kifo cha ghafla cha mbunge huyo na anashindwa kuamini kilichotokea.

Sophia Simba
“Ni msiba mkubwa kwetu, ni jana nilizungumza naye kwa kirefu kuhusu Jimbo la Ukonga kugawanywa, aliniambia kugawanywa ni sawa kwa sababu jimbo lake ni zuri na watu wanampenda,” alisema Sophia na kuongeza:
“Nilikuwa nazungumza naye kwa sababu mimi kama kiongozi wa wanawake (UWT) ninafuatilia sana majimbo yanayowakilishwa na wanawake.”

Grace Kiwelu
“Tumepokea kwa masikitiko taarifa za kifo hicho, jana (juzi) jioni tulikuwa naye. Lakini leo (jana) hii kabla sijaanza kuchangia nilisikia taarifa hizi, nilipata wakati mgumu kuchangia maoni yangu kwa hotuba ya Wizara ya Afya.

James Mbatia
Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia alimzungumzia marehemu Mwaiposa kwamba hakuwa mtu wa kupenda vurugu na alikuwa anawakilisha mambo ya kitaifa na jimboni kwake.
“Alifahamu majukumu ya mbunge kwamba ni kusemea wapigakura na alijua jema ni lipi na baya ni lipi hakuwa na hila, tutamkumbuka kwa kuelezea jambo analoliamini bila woga, jambo ambalo ni sifa kuu ambayo ni kujadili hoja na si matukio,” alisema Mbatia.

Ole Medeye
Mbunge wa Arumeru Magharibi, Godlack Ole Medeye alimwelezea marehemu kuwa ni jirani yake huko Dodoma na walikuwa wanakutana mara nyingi kanisani eneo la Chadulu.
“Ni mwadilifu, mtetezi wa haki na kusimamaia analoliamini. Ninatumia nafasi hii kuwaomba wapigakura wake hususan wana CCM kwamba msiba huo usiwagawe na usiwe mwanzo wa vurugu ndani ya chama. Tuimarishe umoja wetu ili baadaye tumpate kiongozi mwingine mwema,” alisema Ole Medeye.

HISTORIA YA MWAIPOSA
Alizaliwa Novemba 23, mwaka 1960 mkoani Kilimanjaro. Alisoma shule ya Msingi Nkweseto kati ya mwaka 1967 hadi 1974 na baadaye Shule ya Sekondari Masama mwaka 1976 hadi 1980.
Alijiunga na Shinyanga Commercial School (Shycom) mwaka 1981 hadi 1983 na baadaye Chuo cha Eastern & Southern African Management Institute (ESAMI) mwaka 2007 ambako alipata cheti cha uongozi na kati ya mwaka 2006 hadi 2009 alisoma Hanns Seidel ambako nako alitunukiwa cheti cha uongozi.
Kati ya mwaka 1986 na 1992 alipata Shahada ya Uzamili ya International Economic Relations katika Chuo cha Higher Economics Institute ‘Karl Marx’, Sofia, Bulgaria na mwaka 2004 hadi 2007 alipata Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Strathclyde, Glasgow nchini Scotland.
Kwa upande wa kazi, Mwaiposa aliwahi kufanya kazi Tumaini Financial Agency kama mkurugenzi, mwaka 2008 hadi 2010, Kipunguni SACCOS Ltd kwa nafasi ya Mwenyekiti mwaka 2005 hadi 2010, Shule ya Msingi Tumaini kwa nafasi ya Mkurugenzi na Mshauri kati ya mwaka 2005 hadi 2010 na pia alifanya kazi Benki ya CRDB, Tawi la Azikiwe akiwa Msimamizi Mkuu mwaka 1986 hadi 2008.
Kwa upande wa siasa, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwamo Mwenyekiti wa CCM tawi la Kipunguni na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).
Aliolewa na Ally Mwaiposa na kufanikiwa kupata watoto wawili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles