Mbunge wa Siha, Godwin Mollel (Chadema), amesema anakusudia kuwasilisha muswada binafsi bungeni kupendekeza kuwe na Tume Huru ya Uchaguzi ili kuiepusha nchi na umwagaji damu wakati wa uchaguzi.
Amesema kusudio hilo ni kwa sababu mfumo wa sasa wananchi wameshuhudia kila chaguzi kunakuwa na umwagaji wa damu ambapo muswada huo utanusuru Tanzania kuwa kama nchi nyingine.
“Hili jambo la kuwa na tume huru halitakuwa na manufaa tu kwa upinzani lakini pia itaisaidia CCM (Chama Cha Mapinduzi) kwa sababu kama sisi Ukawa tukitumia nguvu kama wanavyotumia wao dola, tutashinda kwa sababu sisi ni wengi kuliko wao.
“Kimsingi hata kama wanatumia nguvu ya dola kwa kiasi kikubwa hakuna nguvu ya dola iliyowahi kushinda nguvu ya umma hasa watu wengi,” amesema Dk. Mollel.
Aidha, Dk. Mollel amesema hata kama kuna umwagikahji wa damu unakuwa ni mdogo ni kwa sababu ya busara ambazo viongozi wa upinzani wanatumia kwamba hata kama wanalazimishwa kufanya jambo fulani wao hawahamasishi watu kujaribu kutumia nguvu katika kufanya hilo jambo.
“Naamini uvumulivu una kikomo sasa kabla hatujafika huko ambapo uvumilivu unafikia kikomo ni vema pakatokea watu wachache ambao watatengeneza mfumo wa Kitanzania ambao utakuwa huru na wa kumridhisha kila mtu ili kuhakikisha Tanzania inapata kile nchi inachotaka badala ya kile ambacho watu wachache wanakitaka,” amesema.