NA ASHA BANI
-DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), amekabidhi madawati 290 yenye thamani ya zaidi Sh milioni 28 yatakayogawanywa katika shule mbalimbali za jimbo lake.
Akikabidhi madawati hayo juzi katika Shule ya Sekondari Mashujaa, alisema amefanya hivyo kutokana na kuona umuhimu wa wanafunzi hao kusoma katika mazingira bora zaidi.
Alizitaja shule zitakazopata mgawo wa madawati hayo kuwa ni shule ya Manzese madawati 30 na viti 30, Makoka madawati 30 na viti 30, Makuburi madawati 30 na viti 30, Mugabe madawati 30 na viti 30, Mabibo madawati 30 na viti 30 na Mashujaa madawati 50 na viti 50.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mashujaa, Edda Kondo, alimwelezea mbunge huyo changamoto iliyopo shuleni hapo kuwa ni pamoja uhitaji wa ukarabati wa vyumba 17.
Pia shule haina maabara za sayansi, vifaa vya sayansi na vitabu.
“Kwa kua shule ni mpya haina vitabu vya masomo yote ya kufundishia na vifaa kama vile chaki , vifaa vya kutengeneza zana za kufundishia kalamu na vinginevyo.
“Tukumbuke Tanzania yetu ya viwanda na teknolojia hivyo tunahitaji vitendea kazi kama vile photocopy mashine, printa kwa ajili ya matumizi ya ofisi kama kuchapisha mitihani na mazoezi ili kupandisha taaluma ya wanafunzi,” alisema Mwalimu Edda.
Alisema shule pia haina ofisi za walimu wanatumia vyumba vya madarasa kama ofisi ambavyo vinahitaji ukarabati na ukosefu wa meza na viti.
Pia alisema shule haina uzio hali inayosababisha kuvamiwa na wahuni au watumiaji dawa kulevya na hata kushuhudia vitendo viovu.
Akielezea idadi ya wanafunzi katika shule hiyo alisema wamefikia 951 wakiwamo wavulana 478 na wasichana 473 , walimu 23 .