28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Kagere aanika siri ya kuiliza Yanga

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MSHAMBULIAJI wa Simba, Meddie Kagere, amesema amekuwa akitumia akili zaidi anapokuwa katika eneo hatari  la wapinzani, hatua inayomfanya kufunga mabao ambayo yamekuwa yanaisaidia timu yake.

Kagere juzi alifunga bao pekee la Simba katika ushindi wa 1-0 dhidi ya mtani wake Yanga, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Bao hilo lilimfanya mshambuliaji huyo wa zamani wa Gor Mahia kufikisha mabao tisa msimu huu akiwa na kikosi hicho cha Msimbazi, akilingana na mpachika mabao wa Alliance, Dickson Ambundo.

Kwa ushindi wa juzi, Simba ilifikisha pointi 39 na kusogea hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikitoka nafasi ya nne baada ya kushuka dimbani mara 16, ikishinda michezo 12, sare tatu na kupoteza mchezo mmoja.

Akizungumza baada ya pambano lao na Yanga kumalizika, Kagere alisema baada ya kufanikiwa kuvuna pointi tatu, kwa sasa wanaangalia mbele kuhakikisha wanafanya vizuri katika michezo yao ijayo.

“Unapokuwa eneo la hatari la mpinzani wako, unatakiwa kuongeza umakini ili uweze kupata kile unachokihitaji, unatakiwa kutumia akili zaidi kuliko nguvu, umri  si kitu sana, mara nyingi napenda kujipa changamoto mwenyewe, licha ya mechi kuwa na ushindani mkubwa nashukuru tumepata pointi tatu muhimu,” alisema Kagere aliyewahi kukipiga  Piliso Rwanda.

Alisema kwa sasa anautazama mchezo wao unaofuata dhidi ya African Lyon, unaotarajiwa kuchezwa kesho Uwanja wa  Sheikh Amri Abeid  jijini Arusha.

Wakati huo huo, kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, amemzungumzia mshambuliaji huyo kwa kusema ni mchezaji tishio anapokuwa eneo la hatari la wapinzani.

“Simba ilicheza kwa kiwango bora kuliko sisi, wachezaji wangu walishindwa kutambua tunahitaji nini, ukiangalia hata bao tulilofungwa mabeki walikosa umakini na kushindwa kutambua pale alikuwepo mshambuliaji wa aina gani,” alisema Zahera.

Kagere ameonekana kuwa mwiba  mchungu kwa mabeki wa timu  mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara na katika michuano ya kimataifa, ambapo Simba inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kabla ya  kuipa ushindi juzi dhidi ya Yanga, Kagere pia aliiongoza Simba kuitungua Al Ahly ya Misri bao 1-0 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pia alionyesha  umahiri wa kupachika mabao wakati Simba  ilipoumana na Mbabane Swallows ya nchini Swaziland, akifunga bao moja Wekundu waliposhinda 4-1 Uwanja wa Taifa kabla ya kufunga idadi hiyo hiyo iliposhinda  4-0 ugenini.

Alithibitisha ubora wake wakati Simba ilipoitungua Nkana Red Devils ya nchini Zambia mabao 3-1, ambao alifunga bao la pili kwa kichwa kabla ya kuifungia mabao mawili Simba ilipopata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya J.S Saoura ya Algeria.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,186FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles