29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge CCM awasilisha bungeni Azimio la kumpongeza JPM, Lema asema anaomba uwaziri

Fredy Azzah, Dodoma



Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu, amewasilisha bungeni azimio la kumpongeza Rais John Magufuli kwa hatua alizochukua juu ya zao la korosho, huku Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, akisema anachofanya Kingu ni kuomba uwaziri.

Kingu akitoa azimio lake alisema kwa muda mrefu bei ya mazao yanayotumika na serikali kama mazao ya kimkakati, yamekuwa yakilalamikiwa na wakulima kutokana na bei yake kuwa ya chini mara kwa mara.

Amesema kutokana na hilo wakulima wamekuwa wakiilalamikia serikali yao wakitaka ichukue hatua za haraka ili kunusuru soko la mazao hayo.

Kingu amesema wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakitoa visingizio mbalimbali ili kutafuta njia ya kuwadhulumu wananchi wanyonge wa Tanzania kwa kigezo cha bei ya soko la dunia.

“Nachukua nafasi hii, kumpongeza Rais John Magufuli, kwa kubaini ujanja na dhuluma hiyo kwa wakulima na kuja na suluhisho la kudumu la kuwakomboa wakulima masikini wa nchi hii,” amesema Kingu.

Amesema mbali ya kubaini udanganyifu huo, Rais Magufuli pia ameweza kutoa miongozo mbalimbali kwa watendaji wa serikali ya namna bora ya kuwatafutia wakulima masoko ya mazao ya ili kuwawezesha kufaidika na nguvu ya jasho lao.

“Jitihada hiyo ya serikali imeanza kuzaa matunda ya moja kwa moja katika kuwainua wakulima ambapo Novemba 12, mwaka huu, Rais Magufuli alitangaza neema kwa walulima.

“Uamuzi wa Rais wa kusitisha ununuzi wa zao la korosho kwa wakulima wa Mikoa ya Kusini kupitia kwa wafanyabiashara na badala yake serikali kuamua kununua kupitia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na fedha kutolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo ni uamuzi wa kihistoria kwa taifa letu,” amesema Kingu.

Amesema uamuzi huo wa Rais Magufuli umeweza kufuta mpango mchafu wa wafanyabiashara waliopanga kununua korosho hizo ghafi kwa Sh 2,500 tofauti na ile ya Sh 3,500 waliyonunua katika msimu wa kilimo wa mwaka 2017 ili kuwaibia wakulima.

Amesema hatua ya Rais Magufuli ya kutoridhishwa na bei hiyo ulimfanya kutangaza bei nzuri ya Sh 3,300 kwa korosho hiyo ghafi, hatua iliyoibua shangwe kwa wakulima si wa zao hilo la Korosho pekee bali kwa wakulima wote wa Tanzania.

Aidha Kingu amesema hatua hiyo ya serikali imewezesha kuokoa zaidi ya Sh bilioni 160 endapo Korosho hizo zingeweza kununuliwa na wafanyabiashara kwa bei ya Sh 2,500.

“Uamuzi huu pia umelenga kuwaondoa wakulima katika unyonyaji wa minyororo ya wafanyabiashara wenye nia mbaya na nchi yetu na ni uamuzi unaoleta tija katika kuwainua wakulima,” alisema Kingu.

Pamoja na kutoa pendekezo la kumpongeza Rais Magufuli, Kingu pia kupitia hoja yake hiyo aliitaka Serikali ichukue hatua za haraka za kutafuta masoko ya mazao mengine yakiwemo Pamba, Kahawa, Mbaazi, Ufuta, Mchele na kuimarisha mpango wa kuongeza thamani ya mazao.

Akichangia katika hoja hiyo, Mbunge wa Viti Maalum, Riziki Rulida (CUF) alisema Rais Magufuli amechukua uamuzi ambao utakuwa historia katika ukombozi wa wakulima wa nchi.

Naye Mbunge wa Nachingwea, Hassan Masala (CCM) alisema Bunge kwa ujumla limefurahishwa na hatua hiyo ya Rais Magufuli imeibua shangwe kwa wakulima wa Korosho wa Mikoa ya Kusini.

Kwa upande wake Lema, alisema; “kama ambavyo ni hali kumpongeza Rais ni halali vile vile kumkosoa, mimi nitajikita kumkosoa, huwezi kuwa unamtafuta uwaziri ama unaibu waziri kwa kiwango kikubwa hiki.

“Biashara duniani inatengenezwa na ‘demand na supply’, leo kungekuwa na kampuni 1,000 zinagombania kununua korosho, unapotumia jeshi gharama za zinazotumika kuanzia usafiri ni hasara kubwa kuliko faida itakayopatikana,” alisema Lema.

Wakati Lema akiendelea, Waziri wa Maliasi la utalii, Hamis Kigwangala, aliomba kumpa taarifa Lema akisema “ukisoma uchumi huwezi kuangalia demand na supply tu, ni lazima uangalie mambo mengine, wakati mwingine hutokea Serikali kuingilia, nilipenda amalizie ‘theory’ zote, ndiyo maana kuna mifumo inayosaidia kuweka uchumi sawa, kudhibiti bei, kununua mazao, inaangalia bei zikiharibika inaweza kuingiza mazao kwenye soko.”

Naibu Spika Dk. Tulia Ackson, alimpotaka Lema kupokea taarifa hiyo, alisema “ukapambane kwanza na suala la kuzuia mashoga uwanja wa ndege pele.”

Lema aliendelea kwa kusema “kwenye suala la korosho, linaenda kuanguka kama kahawa, haiwezekani Waziri Mkuu analeka wateja wa kunua zaidi ya tani 200,000 alafu Rais anasema achana na hao wateja, wanajeshi mkanunue korosho.”

Amesema jeshi linanunua korosho lakini haijulikani haijulikani soko lake litatoka wapi.

Wakati Lema akiendela na hoja yake, Mbunge wa Kasulu Vijijini, Agustino Vuma (CCM), alisimama kumpa taarifa Lema akisema, soko la korosho lipo kubwa na litaanza na Watanzania wenyewe.

Lema alipopewa nafasi ya kujibu taarifa hiyo alisema “siamini jana (juzi) nilikuwa nimekaa naye huyu pale kantini, ndiye alikuwa msitari wa mbele kusema Rais anakosea.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles