23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge CCM ataka Ukawa, Naibu Spika wayamalize

Dk. Tulia Ackson
Dk. Tulia Ackson

Na Arodia Peter, Dodoma

MBUNGE wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwanko (CCM) amemtaka Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, kukaa na wabunge wanaounda vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)  wamalize tofauti zao.

Kauli hiyo aliitoa jana bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa bajeti ya Serikali ya 2016/2017.

Alisema ni vema   Dk. Tulia  kwa kushirikiana na Kamati ya Uongozi wakae na kuangalia namna bora ya kumaliza tofauti hizo ili kuweka sura nzuri ya Bunge.

Mbunge huyo ambaye   aliwahi kuwa mwanachama wa NCCR-Mageuzi na kufanikiwa kushika nafasi ya juu ndani ya chama hicho, alisema   ifike mahali kama kuna mgogoro au malumbano kati ya pande hizo mbili, yamalizike.

Hadi sasa mjadala huo wa bajeti unachangiwa na wabunge wa CCM pekee baada ya wenzao wa Kambi Rasmi ya Upinzani, kususa vikao vyote vinavyoendeshwa na Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson wakidai hawana imani naye.

Wakati  mbunge huyo alipokuwa anatoa hoja hiyo, baadhi ya wabunge wa CCM walimzomea na kumpinga waziwazi huku wengine wakimwambia katumwa na wabunge wa upinzani kuwatetea.

Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM) aliomba kutoa taarifa  na alipopewa nafasi alisema:

“Mheshimiwa Spika nasimama hapa kwa kutumia kanuni ya 67 (7), hakuna mbunge yeyote wa upinzani aliyefukuzwa, kwa hiyo mbunge unapotaka Naibu Spika awasamehe maana yake yeye amewakosea.

“Ukweli ni kwamba hakuna aliyewakosea wao wanatoka humu bungeni kwa amri ya mwenyekiti wao Mbowe (Freeman)” alisema Lusinde.

Baada ya Lusinde kutoa taarifa hiyo, Naibu Spika alimuuliza Nsanzugwanko kama anapokea taarifa hiyo, lakini kabla hajasema kama amepokea taarifa hiyo, alimwomba Naibu Spika alinde muda wake.

“Mheshimiwa Spika, namwelewa sana Lusinde, lakini ninachotaka muelewe hapa sisi ni wabunge wa chama kikubwa, ndiyo wenye bajeti hao wenzetu hata wakitoka bungeni mwaka mzima hawana cha kupoteza sisi ndiyo wenye dhamana, kwani hawa wenzetu tukiwasamehe tunapoteza nini?” alihoji mbunge huyo.

Akitoa ufafanuzi wa suala hilo baada ya mjadala huo, Dk. Tulia alisema wabunge wa upinzani ambao wamesusa vikao vyake hawajamkosea na wala yeye hana kosa lolote kwao.

“Mheshimiwa mbunge kama nadhani wamekutuma uje kuwasemea hapa, unaposema niwasamehe, je, niwasamehe kwani wamenikosea? Wala wao hawana kosa lolote na hawajazuiwa na mtu yeyote kuingia humu bungeni kama uliwauliza na wamekwambia hivyo si kweli.

“Kanuni zetu zimeweka utaratibu, Kanuni ya 5 inampa fursa mbunge nini cha kufanya kama hujaridhika na uamuzi wa Spika, utaratibu huu upo kwenye kanuni.

“Hata hivyo hawa wapinzani unaosema wasamehewe wamepeleka hoja kwenye kanuni, hakuna mahali kanuni zinasema wasuse vikao wakiwa ni wawakilishi wa wananchi,” alisema Dk. Tulia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles