Hadija omary, Lindi
Serikali imeombwa kutoa elimu na kuvisaidia vifaa vya kisasa vikundi vya ulinzi shirikishi wa utunzaji na usimamizi wa rasilimali za bahari (BMU) ili viweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Ombi hilo limetolewa na Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini, Selemani Bungara maarufu Bwege, alipokuwa anazungumza na Mtanzania Digital baada ya kutembelea vikundi hivyo katika maeneo tofauti wilayani Kilwa leo Jumatatu Januari 14.
Bungara amesema uwepo wa BMU umesaidia kupunguza kasi ya uvuvi haramu na kufanya ongezeko la samaki waliopotea kurejea wakiwamo kasa, pono, kolekole na pweza.
Naye Mwenyekiti wa Kikundi cha BMU, Amidu Nassoro, amesema kazi inayofanywa na vikundi hivyo ni kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ndani ya bahari na kuwakamata wavuvi haramu wanaotumia mabomu, kokoro na zana nyingine haramu za uvuvi.
Aidha, Nasoro ameelezea changamoto walizo nazo ni ukosefu wa vitendea kazi ikiwamo boti za kisasa za kufanyia doria na nguo nzito.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai, amesema uwepo wa BMU umechangia ongezeko la samaki hasa maeneo ya Somanga, Songosongo, Kivinje na Masoko.
Amesema Mapato ya halmashauri ya wilaya hiyo yatokanayo na uvuvi yameongezeka kutoka Sh milioni 11 kwa mwezi mwaka 2015 hadi kufikia Sh milioni 25 mwa mwezi mwaka jana.