Anna Potinus, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe, amesema hataondoka katika nafasi hiyo kwa shinikizo la wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) isipokuwa wanachama wa chama hicho wakimtaka aondoke ataondoka.
Mbowe ameyasema hayo leo Jumatano Septemba 19, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ambapo amezungumzia kilichotokea kwenye uchaguzi mdogo wa marudio uliofanyika hivi karibuni na kuelezea msimamo wa chama hicho.
“Hii kazi si nyepesi kama mnavyofikiria ni ya ujasiri wala mtu asifikirie kuna faida kuwa Mwenyekiti wa Chadema huu ni utume, hii kazi ina msalaba ambao sio kila mtu anaweza akaubeba, nimepewa mamlaka na wanachama wangu wakinitaka niondoke hata kesho nitaondoka lakini nikiambiwa na watu walioko CCM siondoki,” amesema.
Pamoja na mambo mengine, Mbowe amesema kelele zinazopigwa na CCM kuhusu wanaohama katika chama chao hazitawaondoa katika reli na kwamba kukimbia kwao hakutawafanya washindwe kwenda mbele
“Kila anapoondoka diwani mmoja kuna wanachama maelfu wanaingia Chadema, wale ambao wana moyo mwepesi wameshindwa kukabiliana na hizi siasa zenye changamoto tunawatakia heri huko wanakokwenda sisi tutaendelea maana wako wanachama wengine wengi tutawaibua utakapofika uchaguzi mwingine ujao”, amesema
Aidha, amesema wanaofikiri kuwa kazi yake ni nyepesi wanakosea na kwamba CCM wasitarajie kuwa ataondoka kutokana na kelele wanazopiga kwani mamlaka hayo alipewa na wanachama wake.
Comment:ahsanteni kwa kutuelimisha japo kwa ufupi kwa mfumo huu!